Ruby atoboa siri kupenda kuimba nyimbo za Beyonce

Msanii Hellen George maarufu kwa jina la Ruby, amesema moja ya sababu ya kupenda kuimba nyimbo za mwanamuziki Beyonce ni kuwa na sauti zinazokaribia kufanana.

Ruby aliyasema hayo alipohojiwa na Mwanannchi kwenye tuzo za malkia wa nguvu ambapo aliwakonga nyoyo watu waliofika kwa kuimba wimbo wa Beyonce uitwao ‘I was Here’.

Hii sio mara ya kwanza katika shoo ambazo amekuwa akialikwa msanii huyo kuimba nyimbo za Beyonce, jambo lilimsukuma mwandishi wa habari hii kutaka kujua sababu ya yeye kufanya hivyo licha ya kuwapo kwa wasanii wengi wa Marekani wanaofanya vizuri kwa upande wa wanawake.

Katika majibu yake Ruby alisema anaamini sauti yake na Beyonce zinafanana ndio maana kila anapoimba nyimbo zake huwanyanyua watu vitini.

“Kama ningekuwa simpatii Beyonce, hakika watu wasingenishangilia wakati nikiimba na kunitunza fedha, ndio maana kila ninapokuwa kwenye shoo lazima niimbe nyimbo zake,” alisema Ruby aliyetumbulishwa kimuziki na wimbo wa ‘Yule’.

Alisema mapenzi yake kwa Beyonce yanaenda mbali zaidi kwani angependa pia kuishi maisha kama yake ikiwamo ya ndoa.

Akifafanua hilo, alisema mwanamuziki huyo na mumewe Jay Z sio watu wa kuanika maisha yao binafsi ya ndoa kwenye mitandao na vyombo vya habari na badala yake wamejielekeza zaidi kutangaza kazi zao.

“Maisha wanayoishi Beyonce na mumewe yananivutia sana natamani tuishi hivyo mimi na baba mtoto wangu Kusa na maisha yetu binafsi kubaki kama picha za ‘behind the scene’” alisema Ruby.

Katika tuzo hizo za malkia wa nguvu, Ruby alichangamsha shughuli pale alipopanda jukwaani na kuimba kwa kutumia muziki wa vyombo nyimbo nne mfululizo, ukiwamo ‘I was Here’ na nyimbo zake kama Alele, Ntade na Yule.

Licha ya kwamba hajamaliza hata siku 40 tangu atoke kujifungua, msanii huyo ameonekana kuwa na pumzi kwenye kuimba jambo analosema limechangiwa na kufanya mazoezi na kutobweteka kisa ni mzazi.

Hii ni mara ya pili kwa Ruby kufanya shoo tangu ajifungue ikitanguliwa na ile ya kuchangia ujenzi wa mabweni kwa shule za Wilaya ya Kisarawe iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City.