Shindano la Miss Universe Tanzania larejea

Tuesday October 8 2019

 

By Seif Kabelele @SeifKabelele

Dar es Salaam. Shindano la kumsaka Miss Universe Tanzania linatarajiwa kufanyika tena mwaka 2019 baada ya kutofanyika mwaka jana.

Warembo 90 wa shindano hilo linaloandaliwa na kampuni ya Compass Communication kutoka mikoa mbalimbali nchini wamefanyiwa usaili kupata wachache watakaoshindana kumpata mshindi mmoja.

Mwaka 2019 shindano hilo litawahusisha warembo 10 kutoka mikoa  ya Mwanza, Arusha, Dodoma na Dar es salaam na linatarajiwa kufanyika Oktoba 12 katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es salaam.

“Urembo ni sanaa na urembo ni kazi na ndiyo maana sisi kama Compass Communications tumeona fursa na kuamua kuendeleza vipaji vya wasichana wengi wenye ndoto na kuamini kuzifikia kupitia tasnia hii ya urembo” amesema mkurugenzi wa Compass Communications, Maria Sarungi Tsehai.  

Miaka ya nyuma, shindano hilo limeibua vipaji vya warembo wengi ambao wameendelea kufanya vyema kwa kupeperusha bendera ya Taifa.

Baadhi ya warembo hao ni Flaviana Matata, Nelly Kamwelu na Hellen Dausen.

Advertisement

Tsehai amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri na wadau wote wa tasnia ya urembo.

“Tunaishukuru sana Serikali, wizara husika pamoja na Baraza la Sanaa (Basata) kwa kutupatia ushirikiano kwa miaka yote ni matumaini yetu kwamba tutazidi kupata ushirikiano na kusogeza kwa pamoja hili gurudumu la sanaa,” amesema Maria Sarungi.
Mbali na shindano hilo la urembo, mwaka 2019 mashindano haya yanaadhimisha miaka 12 tangu kuanza kufanyika hapa nchini mwaka 2007. Mshindi wa shindano hilo ataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia yatakayofanyika mwishoni mwa  mwaka 2019.

 

 

Advertisement