Snura aukumbuka wimbo wake wa Chura, atoa neno kwa wasanii mwaka 2019

Friday December 28 2018

 

By Rhobi Chacha, Mwananchi

Dar es Salaam. Msanii Snura Mushi amewakumbusha wasanii wenzake wanapouanza mwaka 2019 kukumbuka kuna Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) hivyo wnapaswa  kuzisoma na kuzijua sheria zake ikiwamo zinazokata mavazi ya nusu utupu, mashairi ya kukera.

Amesema Basata ipo na ilikuwapo lakini miaka hii miwili wamekuwa makini kufuatilia kazi za wasanii na mienendo yao, hivyo wasanii walitambue hilo ili kupunguza kuingia kwenye malumbano na taasisi hiyo muhimu kwenye tasnia.

Akizungumza na Mwananchi leo, Snura amesema mwaka 2018 umekuwa na matukio mengi ya malumbano kati ya wasanii na baraza hilo, jambo ambalo linapaswa lisijirudie.

“Kama wasiposoma vizuri sheria za baraza ambalo tunapaswa kufanya nalo kazi, watakuwa wanarudia makosa yaleyale, hivyo ni vema wakaenda na wakati kwa kujua wanapaswa kutembea kwenye mstari upi.”

“Kilichonitokea kwenye wimbo wa Chura kilinifundisha ndiyo maana nimebadili mashairi, nguo ninazovaa wakati wa kufanya shoo, lengo likiwa ni kufanya kazi kulingana na matakwa ya mamlaka hiyo inayosimamia wasanii, ”amesema.

Amesema kitu anachokijutia ni mavazi ya nusu utupu aliyokuwa akivaa ambapo akiona picha zake hadi sasa anajisikia alijikosea yeye na jamii iliyokuwa ikimuangalia.

Advertisement