Steve Nyerere amuomba radhi Ommy Dimpoz

Ommy Dimpoz

Muktasari:

  • Siku chache baada ya Steve Nyerere kudai msanii, Ommy Dimpoz hawezi kuimba tena baada ya kufanyiwa operesheni ya koo, leo Jumapili Februari 10, 2019 amemuomba radhi jambo ambalo Dimpoz ameridhia

Dar es Salaam. Siku chache baada ya mchekeshaji, Steven Mengere ’Steve Nyerere’ kudai msanii, Ommy Dimpoz hawezi kuimba tena baada ya kufanyiwa operesheni ya koo, leo Jumapili Februari 10, 2019 amemuomba radhi.

Dimpoz ameuridhia msamaha huo na kumtaka mchekeshaji huyo amuache aendelee kutumia vichekesho vya wachekeshaji wengine, wakiwemo Joti na Dullivan wanaoigiza kuhusu kauli hiyo ya Nyerere.

Steve Nyerere katika moja ya video zilizosambaa mitandaoni anaonekana akizungumzia operesheni hiyo na kubainisha kuwa ni ngumu kwa Ommy Dimpoz kurejea katika uimbaji kwa kuwa koo lake halitakuwa sawasawa.

Baada ya kauli hiyo, watu mbalimbali walimshambulia mchekeshaji huyo wakisema jambo hilo si sahihi.

Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Steve Nyerere ameandika, “Kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mungu, lakini pili nichukue fursa hii kumuomba radhi ndugu yangu Dimpoz kwa namna alivyopokea kauli yangu niliyoitoa dhidi yake.”

“Na zaidi niwaombe radhi Watanzania wote na wapenzi wa sanaa. Binadamu unapoona hapa umekosea busara inatutaka kukiri kukosea nami nakiri kukosea kutokana na ile kauli yangu kwa Dimpoz.”

Ameongeza, “Najua mie niliteleza kusema kwamba Dimpoz hatoimba tena lakini sikuwa na nia hiyo, kwamba natamani Dimpoz asiimbe tena.”

Amesema pamoja na vichekesho mbalimbali vinavyotolewa juu yake anafurahi kwani vinazidi kuupaisha wimbo wa msanii huyo wa Ni Wewe ambao kwa sasa unatamba katika vituo mbalimbali vya redio.

Katika majibu yake, Ommy Dimpoz pamoja na kushukuru wimbo wake kupata watazamaji zaidi ya milioni moja hadi sasa ikiwa ni siku nne tangu autoe Youtube, amesema amemsamehe mchekeshaji huyo.

“Kuhusu kaka yangu Steve Nyerere mimi kama nilivyosema mwanzo sina kinyongo na wewe najua kama binadamu uliteleza na kuna kitu umejifunza na ningependa utambue bado nakuheshimu sana si unajua wewe ndio kiongozi wetu kwenye mambo yetu yale,” amesema Dimpoz.

Kuhusu video za wachekeshaji mbalimbali zenye utani unaomlenga Steve Nyerere, Dimpoz alimtaka mchekeshaji huyo amuache aviweke.