Sylivia Sebastian aingia 20 bora ya vipaji Miss World 2019

Muktasari:

Inawezekana kiu ya Watanzania kufanya vizuri kwenye mashindano ya urembo ya dunia ikapata suluhisho baada ya mlimbwende wa Tanzania  mwaka 2019, Sylivia Sebastian  kufanya kweli kwenye shindano hilo.

Dar es Salaam. Inawezekana kiu ya Watanzania kufanya vizuri kwenye mashindano ya urembo ya dunia ikapata suluhisho baada ya mlimbwende wa Tanzania  mwaka 2019, Sylivia Sebastian  kufanya kweli kwenye shindano hilo.

Sylivia ameingia 20 bora katika kipengele cha vipaji kati ya washiriki 120 wa shindano hilo kubwa la urembo duniani.

Mwaka 1994 mlimbwende, Aina Maeda ndio alifanikiwa kuingia 20 bora katika kipengele hicho na tangu wakati huo hakuna Mtanzania aliyefanikiwa kuingia katika hatua hiyo.

Kupitia ukurasa wa Instagram wa mrembo wa Tanzania wamempongeza Sylivia kwa kufikia hatua hiyo.

“Kati ya nchi 120 zilizoshiriki Tanzania imo kwenye 20 bora ya nchi zenye vipaji duniani kwenye mashindano ya urembo ya dunia 2019. Hongera sana Sylivia hata kwa hapo ulipofikia umetuletea heshima Tanzania kuwa katika nchi duniani zenye vipaji na sisi tupo.”

 “Warembo wajao wamepata pa kuanzia na kuendeleza ulipofikia umetuweka kwenye ramani, umeweka rekodi mpya mafanikio ni hatua hivyo tangu 1994, 2019 ndio tumefanikiwa kuingia kwenye kipengele hiki cha vipaji. Tunaendelea kukutakia heri kwenye fainali ya Desemba 14.”

Sylivia ameingia 20 bora baada ya kuonyesha ustadi mkubwa wa kucheza ‘Robot Dance’.