TID akerwa kuitwa msanii mkongwe

Muktasari:

  •  Msanii wa Bongofleva nchini Tanzania, Khalid Mohamed TID akiwa na wasanii wenzake, Mandojo na Domokaya wametembelea Ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam na kusema hawapendi kuitwa wakongwe.

Dar es Salaam. Msanii wa Bongofleva nchini Tanzania, Khalid Mohamed ‘TID’ amesema anakerwa na tabia ya baadhi ya watu kuwaita wasanii wa enzi zao kuwa ni wakongwe.

TID ameyasema hayo leo Jumatano Novemba 12,2019 katika mahojiano maalum alipotembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam akiwa ameambatana na wasanii wenzake Mandojo na Domokaya.

Akizungumza kwenye kipindi cha MCL Extra msanii huyo aliyewahi kutamba na kibao cha ‘Zeze’ na ‘Nyota yangu’ amesema kuwaita wao kuwa ni wasanii wakongwe ni kutaka kuwatenga na muziki wa kizazi kipya jambo ambalo anaona si sawa.

“Mnatuitaje wakongwe wakati muziki huo hauna hata miaka 40 hivyo unaposema muziki wa kizazi kipya na sisi tupo ndani yake.”

“Maana ya muziki wa kizazi kipya ni muziki wa sasa, sasa iweje wasanii wake waitwe wakongwe hizo ni chuki na sumu ambazo watu wanataka kuzieneza ili kututenga na muziki huo,” amesema TID

“Kwani sisi wote ni wasanii tunaotakiwa kupewa haki sawa kuanzia kwenye malipo na upatikanaji wa kazi zake,” amesema msanii huyo huku akiungwa mkono kauli yake hiyo na Mandojo na Domo Kaya.

Pia, wasanii hao wamesema katika kuunganisha nguvu kusukuma muziki wao wameamua kuunda umoja wao,  ambao watakuwa wakifanya kazi kama timu huku moja ya kazi wanayoiandaa ni kuandaa tamasha lao  kwa kuzunguka mikoa mbalimbali hapa nchini.