Wakati Nandy anatikisa Fiesta wabongo hawajui Vannesa Mdee alipo

IMEONDOKA wikiendi ya matukio. Anthony Joshua kumbamiza Andy Ruiz na kurudisha mikanda yake. Fiesta ilijimwambafai viwanja vya Uhuru. Wabunge wa kitaa, Luqman Maloto na Dk Levy wapo kikaoni muda huu.

LUQMAN: Una tabia ya kuchelewa vikao. Miaka 58 ya Uhuru bado mtumwa wa muda, mtumwa wa usingizi. Jitahidi uumudu usingizi na uutawale muda

DK LEVY: Bado nina hisia za utumwa wa kiutu na kihisia toka kwa Waingereza? Ndo unachotaka kumaanisha? Kijana hebu kuwa na adabu kidogo ili dhambi zingine zikupitie mbali. Ndo maana Fiesta hujaalikwa.

LUQMAN: Ni kawaida yangu tangu na tangu, nisipoalikwa najialika mwenyewe. Unafiki pembeni, wale jamaa waliiandaa vizuri shoo yao, ila waoga sana. Kiingilio Sh3,000 kweli? Mbona hata mwendo wa tembo mwekundu watu wangejaa? Au wewe usingetoa red elephant kwa ile burudani ya Uwanja wa Uhuru?

DK LEVY: Hata wakifanyia uani kwangu zile makitu huwa sihudhurii siku hizi. Umri baba. Nyakati zimeshapita kwa upande wangu. Mara ya mwisho nilienda mwaka 2003 shoo ilifanyika kule Wet “N” Wild Water Park Kunduchi. Nakumbuka wakati ule Mandojo na Domokaya wa moto kama tairi ya ndege inayotua na ngoma yao ya Nikupe. Ngwair ndo anatoka na Geto Langu. Papii Kocha hagusiki na Sea. Baada ya hapo nikaenda shoo ya Sean Paul pale Diamond Jubilee mwaka 2004. Nadhani sijawahi kuwa mpenzi wa makelele baada ya hapo. Hakuna kitu kinakera kama neno “Niendelee au nisiendelee?” au mwingine hajaanza hata kuimba anaanza kuwaamrisha watu waliotoa pesa eti “Piga keleleeeeee.” Huo umbweha ndo uliniondoa mzuka wa kwenda kwenye shoo zao. Nikashangaa mpaka juzi hapo bado kuna wanamuziki wana hizo swaga za kipuuzi za “Sisikiiii piga keleleee.”

Huu ni ujinga na uharibifu wa muda. Piga shoo kali imba ‘laivu’ au juu ya ‘msidii’ wako lakini wape kitu watu wanataka kisha waache wao ndo wapige kelele au waseme endelea au usiendeee. Mtu mwingine aliyetakiwa kuchukua point kubwa ni Ferouz kwenye shoo ya Wasafi. Akaacha kuimba ngoma zake kiutulivu yeye akaanza kurukaruka muda mwingi suruali ipo chini ya makalio na kuwalazimisha watu wapige kelelee. Wakati ngoma zake nyingi za kusikiliza zaidi na kuelewa. Unawavaliaje suruali chini ya makalio watoto waliozaliwa baada ya ngoma ya Maji ya shingo na Kamanda?

Waendaji wa shoo kwa sasa sio wadogo zetu ni watoto na wajomba zetu. Mtazame Paula yule kisha kumbuka wakati kina Nature wanakwenda kwa Majani pale Bamaga alikuwa na umri gani na sasa ana umri gani? Fiesta juzi nimetazama kwenye runinga nilipoona Ruby kapania badala ya kudhamiria kwa kuanza kupiga makelele badala ya kuimba. Nikaona hapa kutiana ‘stress’ nikaachana nao. Haya leta ujinga wako mwingine nakusikiliza.

LUQMAN: Sikuelewi ujue, unaiponda Fiesta au unaisifia? Tatizo la kupenda supu ya uyoga linakuathiri sana.

DK LEVY: Kiasili wenyeji wa Ujiji wabishi sana. Kama hana bifu na mtu basi hutaka kulazimisha mtu mwingine awe na bifu na mtu. Sasa unachofanya unalazimisha niwe na bifu na Fiesta au na baadhi ya wasanii waliotumbuiza Fiesta? Haya nichagulie wa kujenga naye bifu rasmi tamasha la Fiesta au wasanii waliotumbuiza kama wana mdondo?

LUQMAN: Ali Kiba kapiga shoo kali sana. Kama kawaida yake. Harmonize katisha. Fid Q balaa yule mtu. Mr Blue huwa anapenda sana sifa jukwaani. Prof Jay ameonesha ng’ombe huwa hazeeki maini. Yule Nandy moto wake unazidi kuchochea. Noma kipeo cha pili. Wewe uliyekosa Fiesta kafie mbali.

DK LEVY: Asante kwa kunijulisha kuwa Nandy katisha. Maana moyo ulikuwa unanienda mbio sana kujua kama haka kabinti kamefanya kweli au? Kama Nandy kakimbiza sana basi na Fiesta idumu milele. Muziki wa sasa bila Nandy ni kama soka la Tanzania bila Samatta. Kuna Nandy kisha yupo Nandy na anafuata Nandy ndo unaweza kuendelea na wengineo. Nandy katumwa kufanya muziki yule binti aiseee. Kitoto kimejaaliwa kila kitu. Unajua bana mimi nachelewa kuoa kwa vitu vingi sana. Wanaostahili kuolewa na mimi wanakuja wakati ambao siyo muafaka. Huyu Nandy angekuwepo wakati ule nikiwa sehemu ya wapokeaji wa pesa za EPA ningemuoa mara tatu. Unaelewa maana ya kuoa mara tatu? Yaani zile talaka tatu zingefutwa rasmi kwa maana kuwa asingeachika daima dumu. Nani aoe chawa bana. Watu tunaoa madini tupu.

LUQMAN: Nashangaa muziki, Nandy anastawi, Vanessa Mdee anaondoka. Leo hii Nandy anaweza kufanya matamasha na kujaza lakini Vanessa sina hakika kama hata anaweza kufunga pale Maisha. Natamani niwashindanishe Next Door Arena, mmoja afanye leo, mwingine kesho, nina hakika Nandy atamburuza vibaya Vanessa ambaye wewe unampenda sana.

DK LEVY: Sijakuelewa. Au pengine unajadili haya ukiwa chini ya mtutu wa bunduki. Unajua usipende kujadili vitu ‘siriasi’ ukiwa bado na madeni kabla ya X-mass. Hii hufanya ubongo ukose hewa nyumbulifu na kujikuta muda mwingi unatoa maneno ambayo ni dhahiri shahiri unatafuta sababu za kutandikwa makofi mkurabita. Na nitakutandika muda siyo mrefu. Nandy ni wa kwetu ila Vanessa Mdee ni wa kwao.

Najua huwezi kuelewa bado hapa. Ni kwamba Vanessa aliumbwa kwa ajili ya watu wa mataifa. Nandy aliumbwa kwa ajili ya taifa. Hivi lugha inayotumika mara nyingi kwenye kinywa cha Vanessa unadhani ataeleweka na shangazi zako wa Akachube Road? Vanessa anaeleweka huko alikobeba tamaduni zao. Kifupi Vanessa hawezi kujaza hata daladala la Gongo la Mboto akiamua kufanyia shoo kwenye DCM. Watu hawamuelewi ila dunia inamtambua. Next time usipende kumfananisha Nandy na hao nanii zako. Tuheshimiane mzee.

LUQMAN: Sasa hapo unamaanisha nini? Huko ambako Vanessa anaeleweka mbona hatuoni mambo? Diamond tunamuona anavyotoboa kimataifa. Vanessa kweli kuna kipindi alitoboa, ila sasa hatuoni kitu. Lini Vanessa amewahi kujaza peke yake shoo ya watu 300 nje ya Bongo? Tuanzie hapo?

DK LEVY: Tafsiri ya kueleweka ni tofauti na tafsiri yako unayotaka au kulazimisha niseme. Aina ya muziki wa Vanessa unaeleweka nje ya mipaka. Sio kwamba unakubalika nje ya mipaka. Bogas wewe. Kaulize ana tuzo ngapi na zote kachukilia wapi? Halafu siku hizi mbona unakwepa sana mijadala ya soka?

LUQMAN: Naona wachezaji wa Yanga wanaandika barua za kuvunja mikataba kama wale jamaa waunga juhudi, kunani huko uliposimama?

DK LEVY: Unajua kushabikia au kufuatilia taarifa za timu ambayo ilikataa uwekezaji, na sasa wanaumia na uwekezaji wa mtu kwa watani wao, ni tatizo kubwa sana. Mzee Akilimali hayupo ‘levo’ za Mzee Kilomoni.

Kwanza Mzee Kilomoni alichezea Simba na alishiriki kujenga majengo ya Simba. Lakini watu wa Simba hawakutaka kumchekea hata kidogo pale alipotaka kuleta zengwe MO asipewe timu. Lakini Mzee Akilimali hata asili ya ukoo wake siyo watu wa mpira. Ni watu wa maneno mengi tu kwenye vijiwe. Hizi timu mwanzoni zilikuwa kama vijiwe tu vya kahawa na soga. Jengo la Yanga lilijengwa na Mzee Karume. Yeye ameendelea kuwa Yanga kama mwanachama tu. Lakini ajabu watu wa Yanga wakamsikiliza ili Manji asipewe timu. Kwa hiyo kama wachezaji wanavunja mikataba waambie Mzee Akilimali akawalipe yeye si ndo mwenye timu?