Wasanii wa rap washtua tuzo Grammy, Watanzania waibuka

Wakati wanamuziki wa Marekani wakijumuika kupongezana kwa mafanikio yao ya mwaka uliopita, yakitawaliwa na muziki wa rap, Watanzania wamesema kuna umuhimu wa kurejesha utamaduni wa kupeana tuzo.

Tamasha la Tuzo za Muziki la Kilimanjaro lililoanzishwa kwa ajili ya kuenzi mafanikio ya wasanii wa Tanzania, halijafanyika kwa miaka kadhaa sasa baada ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kuacha kudhamini kwa kutumia bia yake ya Kilimanjaro Lager.

Kwa mwaka wa 61 mfululizo, taasisi ya Recording Academy usiku wa kuamkia jana iliendesha tuzo za muziki za Grammy kwa kutuza wanamuiziki wa miondoko mbalimbali, huku muziki wa rap ukitamba kwa mara ya kwanza kwa kutoa tuzo nyingi.

Katika tuzo hizo zilizofanyika ukumbi wa Staple Center, nyota wa miondoko ya rap, Card B alikuwa msanii wa kwanza wa kike kushinda tuzo ya “Albamu Bora ya Rap”, wakati Childish Gambino alishinda tuzo nyingine mbili kubwa za “Rekodi ya Mwaka” na “Wimbo wa Mwaka”.

Tuzo ya Rekodi ya Mwaka hutambua wasanii, watayarishaji na wahandisi waliochangia katika kurekodi wimbo ulioshinda, wakati Wimbo wa Mwaka hushughulika na utunzi wa wimbo na hivyo tuzo huenda kwa aliyeuandika.

“Kitendo cha Card B kushinda kama rapa bora kimedhihirisha kuwa wanawake nao wanauweza muziki huu,” alisema Chemical ambaye jina lake halisi ni Claudia Lubao.

Chemical alisema ni wakati sasa wa Watanzania kuwaunga mkono wanawake wanaofanya muziki huo tofauti na awali walipokuwa wakichukuliwa kama wahuni.

“Kama Card B kaweza kuwapiga chini wasanii wakubwa wa kiume katika muziki huo na kuukwaa ushindi, ni wazi hakuna linaloshindikana kwa mwananmke, kikubwa ni support (kuwaunga mkono) tu ya mashabiki. Naamini hata yeye kafika hapo kwa ajili ya watu kumpa ushirikiano katika kazi zake,” alisema msanii huyo.

Naye Rosa Ree alisema ushindi wa Card B, umeonyesha namna gani mlango umefunguliwa kwa wanawake kufanya muziki wa rap.

Rosa Ree, ambaye jina lake halisi ni Rosary Robert, alisema anaamini kilichompa ushindi Card B ni kujituma kwake, jambo ambalo wasanii wa kike walio katika muziki huo wanapaswa kuliiga ili wafike mbali.

Hata hivyo, Rosa Ree alisema inasikitisha kuona hadi sasa nchi haina tuzo kwa ajili ya wasanii licha ya kuwa tasnia hiyo imekua kwa kiasi kikubwa.

Alisema tuzo husaidia wasanii kujipima wapi walipo na wafanye nini, hivyo aliwashauri wadau mbalimbali kujitokeza kuandaa tuzo za muziki ambazo si tu zinawasaidia kupata zawadi, bali hata kuonyesha kuwa jamii inafuatilia na kukubali kazi zao.

Msanii mwingine, Whoze (Oscar Helo) anayetamba na wimbo wa “Huendi Mbinguni”, alisema tuzo ni jambo muhimu kwa wasanii kwa kuwa huwasaidia kujipima uwezo wao.

Alisema kutokana na kukosekana kwa tuzo hizo, wasanii wamekuwa wakitoa nyimbo ilimradi kukimbizana sokoni bila ya kutanguliza suala la viwango.

Alisema tuzo ndizo zinazochangia kumkutanisha msanii na wadau mbalimbali wakiwamo wa ndani na nje ya nchi.

Jijini Los Angeles, California ilikuwa ni shangwe kwa wasanii wa hip-hop, wanawake na pia Wamarekani weusi.

Kwa mwaka wa pili mfululizo, wasanii weusi wa miondoko ya hip-hop walitawala hafla hiyo.

Hata hivyo, tofauti na miaka iliyopita, safari hii wasanii hao weusi walishinda tuzo kadhaa kubwa, labda ikiwa ni ishara kuwa taasisi inayoandaa tuzo hizo ya Recording Academy inaanza taratibu kuzoea utamaduni wa muziki wa pop.

Ushindi wa Cardi B uliotokana na albamu yake ya “Invasion of Privacy (kuingilia faragha)” ulikuwa ni kuvisha taji mafanikio ya msanii huyo ambaye sasa anatawala chati za muziki wa hip-hop unaotawaliwa na wanaume.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26, aliwashinda Mac Miller na Travis Scott alipotwaa tuzo hiyo ya kwanza kwake ya Grammy katika maisha yake ya muziki, akiwa ameanza kuchomoza na kibao kilichotamba cha “Bodak Yellow”.

Akionekana dhahiri kutetemeka, na akiwa ndio kwanza ametoka kutumbuiza kibao chake cha “Money kwenye hafla hiyo,”, Cardi B alitoa hotuba ya kushukuru iliyokuwa na hisia akiwa pamoja na mumewe, Offset wa kundi la wasanii watatu wa rap la Migos.

“Neva ni mbaya sana. Labda nianze kuvuta bangi,” alisema msichana huyo huku akicheza, kabla ya kumgeukia Offset na kusema: “Wewe mume, asante.”

Mvuto wa Cardi B unaonekana kwenye albamu nzima, ambayo inaelezea jinsi alivyopanda chati katika muziki.

Nyota huyo mzaliwa wa Belcalis Almanzar alitoa nyimbo kwa ajili ya filamu wakati wa majira ya joto mwaka 2018 kutokana na kibao chake cha “I Like It,” ambacho kinaenzi asili yake ya Amerika Kusini kwa kuweka viwango vya boogaloo vya miaka ya sitini.

Katika moja ya albamu zilizokuwa na mafanikio makubwa mwaka 2018, taasisi inayounganisha wasanii wanaorekodi muziki ya Amerika (Recording Industry Association of America) ilipitisha nyimbo zote zilizo katika albamu ya “Invasion of Privacy” kuwa zilifikia kiwango cha “dhahabu” au juu zaidi.

Hiyo inamfanya Cardi B kuwa msanii wa kwanza wa kike wa muziki wa rap kufikia mafanikio makubwa katika mauzo ya albamu hiyo.

Gambino atamba

Childish Gambino alitwaa tuzo mbili za Rekodi ya Mwaka na Wimbo wa Mwaka, ikiwa ni mara ya kwanza kwa msanii wa rap kupata mafanikio hayo.

Gambino alikuwa mmoja wa wanamuziki waliong’ara usiku wa kuamkia jana, akiwa ameshinda tuzo nne, nyingine zikiwa ni ya kurap vizuri (Best Rap/Sung Performance) na Video Bora ya Muziki kutokana na kibao chake cha “This Is America.”

Hata hivyo, hakutokea kwenye tamasha hilo kufurahia mafanikio hayo.

Drake alishinda tuzo ya Wimbo Bora wa Rap kutokana na kibao chake cha “God’s Plan,” ushindi wake pekee licha ya kutajwa kuwania tuzo saba.

Rapa huyo wa Canada ambaye alikuwa na mzozo na Recording Academy huko nyuma alijitokeza kupokea tuzo yake licha ya kuenea uvumi kuwa asingetokea.

Kendrick Lamar, ambaye aliongoza kwa kutajwa kuwania tuzo nane, alipata ushindi wake wa kwanza katika usiku huo kutokana na kibao chake cha “King’s Dead,” ambacho ameimba pamoja na Jay Rock, Future na James Blake.

Nyota wa muziki wa R&B, Alicia Keys ndiye aliyesherehesha tamasha hilo, na alilianzisha kwa kishindo akiwatambulisha rafiki zake, akiwamo Michelle Obama, ambaye ni mke wa rais aliyepita wa Marekani, Barack Obama.

Obama alifurahisha wageni waliohudhuria wakati alipopanda jukwaani na Keys, Lady Gaga, Jennifer Lopez na mcheza filamu, Jada Pinkett-Smith kutoa ujumbe kuhusu kukubali tofauti na kuwasaidia wanawake.

Brandi Carlile ambaye aliongoza mwaka huu kwa kutajwa kwenye tuzo nyingi, alishinda tuzo zake tatu za kwanza za Grammy.

Nyota wa pop, Gaga alishinda tuzo ya Tumbuizo Bora la Wawili la Muziki wa Pop kutokana na kibao chake cha “Shallow” ambacho kinainogesha filamu ya “A Star Is Born.”

“Najivunia sana kuwa sehemu ya filamu inayozungumzia masuala ya afya,” alisema Gaga akibubujikwa na machozi. Pia, alimshukuru Bradley Cooper aliyeshirikiana naye katika wimbo huo.