Watoto wawagaragaza Wema, Gabo tuzo za SZIFF

Sunday February 24 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Flora Kiyombo (11),  amewaduwaza mamia ya waliohudhuria tuzo za Filamu Zetu International Festival Film (SZIFF) mwaka 2019 baada ya kushinda tuzo ya msanii bora wa kike na kuwabwaga waigizaji wakongwe akiwemo mlimbwende wa Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu.

Wakati Wema aliyekuwa msanii bora wa kike mwaka 2018 akishindwa na mtoto huyo, Rashid Msigala (10) amemshinda Gabo aliyekuwa msanii bora wa kiume mwaka 2018.

Hafla ya utoaji wa tuzo hizo ilifanyika usiku wa kuamkia leo Jumapili Februari 24, 2019 jijini Dar es Salaam huku Flora ambaye hakutegemewa na wengi akiibuka mshindi kupitia filamu ya Kesho.

Filamu hiyo imetengenezwa na kituo cha kulea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu cha Tag Lwang’a  Student Center kilichopo mkoani Iringa.

Mbali na Wema, kipengele cha msanii bora wa kike kilikuwa na wasanii wengine wakongwe, Monalisa na Johari.

Flora aliwataka walioshindwa kufanya vyema mwaka 2019 kujitahidi ili waweze kuibuka na ushindi katika tuzo zijazo.

Baada ya kutangazwa mshindi Flora alikabidhiwa mfano wa hundi ya Sh5milioni.

Kwa upande wake Msigala aliwashinda Gabo na Hemed Suleiman aliokuwa akiwania nao kipengele cha msanii bora wa kiume kupitia filamu ya Kesho aliyocheza sambamba na Flora.

Akizungumzia ushindi wa Flora, Wema amesema amewapa changamoto ya kufanya vizuri zaidi mwaka 2020.

"Siku zote asiyekubali kushindwa si mshindani. Ilikuwa lazima mshindi awe mmoja. Ametushinda mtoto ila kamwe haiwezi kunirudisha nyuma maana watu wananijua mimi ni mkali wao katika filamu hiyo haina ubishi,” amesema Wema.

Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji, Elia Mjata, amesema ushindi wa watoto hao umefungua fursa ya kuzalisha vipaji vipya.

Amesema hata waliowashirikisha watoto hao kucheza filamu hiyo hawakufikiri kama kuna siku watapata tuzo kubwa.

 

Advertisement