VIDEO: Waziri aipa mwezi mmoja kampuni ya Benchmark kumlipa fedha mshindi wa BSS

Naibu Waziri, Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza akizungumza wakati wa Mkutano na waandishi wa jijini Dodoma leo kuhusiana  na Mshindi wa shindano la BBSS Mwaka 2019, Meshack Fukuta (kulia) kutopewa zawadi yake ya Sh Milioni 20 na waandaaji wa shindano hilo Kampuni ya Benchmark. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inchini Tanzania imeipa mwezi mmoja kampuni ya Benchmark 360 ltd kumlipa fedha zote Meshark Fukuta ambaye ni mshindi wa shindano la kusaka vipaji vya uimbaji la BSS mwaka 2019.

Dodoma. Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania imeipa mwezi mmoja kampuni ya Benchmark 360 ltd kumlipa fedha zote, Meshark Fukuta ambaye ni mshindi wa shindano la kusaka vipaji vya uimbaji la BSS mwaka 2019.

Imesema fedha hizo zinatakiwa kulipwa ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo Jumatano Aprili 8, 2020. Fukuta alitakiwa kulipwa Sh20 milioni tangu mwishoni mwa 2019 lakini amelipwa Sh1 milioni tu.

Kampuni hiyo iliyoendesha  shindano hilo imetakiwa kutekeleza agizo hilo kwa muda ulitolewa vinginevyo itafungiwa kusimamia na kuendesha shindani hilo maarufu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma leo naibu Waziri wa Wizara hiyo,  Juliana Shonza amesema tangu kampuni hiyo hadi leo haijaonyesha ni lini watampatia Fukuta zawadi yake.

Shonza amesema  kutokana na hayo serikali imelazimika kutoa maagizo mbalimbali ikiwamo kutoa mwezi mmoja kampuni hiyo kuhakikisha inamlipa mshindi fedha zake.

Hata hivyo, amesema kampuni hiyo ihakikishe  inamtengenezea Fukuta nyimbo pamoja na kumfanyia promo ya kutosha katika kipindi kisichozidi miezi miwili kuanzia jana.

Amesema idara ya sanaa kwa kushirikiana na Baraza la sanaa Tanzania (Basata) wahakikishe kampuni hiyo inawasilisha wizarani nakala ya mikataba ya washiriki waliofika hatua ya 10 bora ya BSS ndani ya wiki moja kuanzia leo..

“Katika shindano hilo Benchmark waliahidi kumlipa mshindi wa mwaka 2019 kiasi cha Sh50 milioni, ambapo Sh30 milioni zingetumika kutengenezea kazi za muziki na kumpromoti mshindi kwa kipindi cha mwaka mmoja na Sh20 milioni angepatiwa. Fainali ilifanyika Desemba 24, 2019 zaidi ya miezi mitatu sasa, mshindi amepatiwa kiasi cha Sh1 milioni tu kati ya zile anazotakiwa kupatiwa,” amesema Shonza.

Kutokana na hayo Shonza ameitaka Basata kuhakikisha inasimamia vyama utaratibu wa waandaaji wa mashindano mbalimbali kukabidhi zawadi za washindi kabla ya siku ya shindano husika.

“Na mara baada tu ya mashindano kumalizika washindi wanatakiwa kukabidhiwa zawadi zao ili kuepusha malalamiko kutoka kwa washiriki, pia wahakikishe wanasimamia utaratibu wa kuwepo kwa mikataba baina ya wasanii na kampuni zinazoendesha mashindano hapa nchini,” alisema Shinza.

Amesema  ni kosa kwa kampuni au taasisi kufanya kazi na wasanii bila kuwa na mkataba huku akiwataka wasanii kutokubali kufanya kazi bila mkataba.

Shonza amesema kabla ya kufikia uamuzi wa kutoa maagizo hayo wizara ilifanya mawasiliano na uongozi wa kampuni hiyo ambapo walisema kuwa wanaendelea na utaratibu wa kumtengenezea Fukuta nyimbo na tayari wimbo mmoja umeshatengenezwa.

Naibu waziri huyo amesema  kuwa wimbo huo hauna ubora unaotakiwa na hivyo wapo kwenye mchakato wa kutengeneza nyimbo nyingine ingawa kuna ucheleweshwaji na sitofahamu kwenye mchakato huo.

“Walisema wameshindwa kumlipa Meshark kwa wakati kutokana na kucheleweshewa malipo ya udhamini wa mashindano kutoka kwa wadhamini wa BSS 2019 kampuni ya Startimes. Wizara ikawasiliana na uongozi wa Startimes na wamekiri kulipa  fedha ya udhamini kampuni ya Benchmark tangu mwezi Januari   2020” amesema.

Alipoulizwa kuhusu madai hayo, mkurugenzi wa kampuni hiyo,  Rita paulsen alijibu kwa kifupi, “nipo msibani niache kwanza.”