Wimbo Uno wa Harmonize waondolewa Youtube, walioutayarisha wazungumza

Muktasari:

  • Wimbo Uno wa msanii wa Tanzania, Rajab Abdul maarufu Harmonize umeibua utata na kuondolewa katika mtandao wa Youtube.

Dar es Salaam. Wimbo Uno wa msanii wa Tanzania, Rajab Abdul maarufu Harmonize umeibua utata na kuondolewa katika mtandao wa Youtube.

Umeondolewa na Magix Enga, mtayarishaji wa muziki nchini Kenya anayedai kuwa mdundo wa wimbo huo uliotoka takribani mwezi mmoja uliopita, ni wake.

Novemba 17, 2019  Enga alimuomba Harmonize kuufuta wimbo huo katika mtandao huo na kumpa wiki moja na kuahidi kuwa asipofanya hivyo, atachukua jukumu hilo mwenyewe.

Enga amesema mdundo wa wimbo huo umefanana na wimbo wa Dundaing alioutengeza.

Mwananchi lilimtafuta Harmonize na meneja wake kuzungumzia suala hilo bila mafanikio kutokana na simu zao kutokuwa hewani huku watayarishaji wa wimbo wa Uno, Hunter na Bonga wakitoa maoni tofauti kuhusu suala hilo.

“Mimi nilifanya ‘mixing’ za huo wimbo, kuandaa mdundo alifanya Hunter G, muulize yeye ndio ana majibu mazuri ya suala hilo,” amesema  Bonga.

Kwa upande wake Hunter amesema, “sijawahi kuiba mdundo wa wimbo wowote katika maisha yangu. Midundo huwa inafanana kwa kuwa unaweza kutumia kinanda au kifaa chochote.”

“Ninachojua mdundo wa wimbo wa Uno nimeutengeneza mwenyewe sijachukua kwa mtu yeyote. Nimefanya kazi nyingi za kuwatengenezea wasanii midundo ya nyimbo zao kama Juliana Kanyomozi, Bushoke na Christian Bella.”

Katika ukurasa wa Instagram wa moja ya meneja wa Harmonize Sebastian Ndege maarufu kama Jembe ni Jembe ameeleza kinachoendelea

"Tumepata Taarifa kutoka Youtube Kwamba,mtu mmoja ambae Inasemekana Kutoka Nchi jiraninya Kenya,Ametuma Barua pepe kudai umililiki wa wimbo wetu Pendwa #UNO.
Aidha kwa taratibu zao YouTube Ni Lazima wauweka Private wakati wakiendelea na taratibu za Kujirdhisha juu ya madai hayo.
Kama Menagement ya @harmonize_tz Tayari tumesha waelekeza Wataalam wetu wa kisheria kufuatilia jambo hili
Kwa kina.

Tunachukua Nafasi hii Kuwaomba Mashabiki wetu na wapenzi wa Harmonize,Kuwa Watulivu Wakati jambo hili linashughulikiwa. Aidha Tunaimani Wimbo wetu Utarudi baada ya muda sio mrefu.Tunawashukuru kwa sapoti yenu.Mungu Awabariki.Asanten sana.
BY HARMONIZE MANAGEMENT #AfroEast #UNO"

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi