Wimbo wa Uno wa Harmonize warejeshwa youtube, aliyeuondoa aupigia debe

Muktasari:

Wimbo wa Uno wa msanii wa Tanzania, Rajab Abdul maarufu Harmonize umerejea You Tube huku aliyehusika kuufungia akiupigia debe watu kuusikiliza na kuuangalia.

Dar es Salaam. Wimbo wa Uno wa msanii wa Tanzania, Rajab Abdul maarufu Harmonize umerejea.

Novemba 20 , 2019 wimbo huo ulionekana kuondolewa katika mtandao wa Youtube baada mtayarishaji wa muziki nchini Kenya, Magix Enga, kudai ni mdundo wa wimbo wake wa Dundaing.

Kutokana na hilo, Novemba 17, 2019  Enga alimuomba Harmonize kuufuta wimbo huo katika mtandao huo kwa kumpa wiki moja na kuahidi kuwa asipofanya hivyo, angechukua jukumu hilo mwenyewe na hata ulipopotea alikiri kuhusika na hilo.

Hata hivyo, leo Jumatatu Novemba 25, 2019 wimbo huo umeonekana kurejea huku Enga akiwa mmoja wa watu anayeupigia debe watu wauangalie na kuusikiliza.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Enga ameandika, “Kila mtu aseme Uno, sasa unapatikana youtube katika audio na video.”

Hata hivyo, Mwananchi imeutafuta uongozi wa Harmonize kuweza kujua kimetokea nini hadi ukarudishwa kwani waliahidi kufuatilia wakati ulipofungiwa lakini simu zao ziliita bila kupokelewa.

Katika taarifa hiyo iliyoandikwa na moja wa meneja wa Harmonize ilisema, “Tumepata Taarifa kutoka Youtube kwamba, mtu mmoja ambaye inasemekana kutoka nchi jirani ya Kenya, mmetuma barua pepe kudai umiliki wa wimbo wetu pendwa wa UNO.”

Aidha kwa taratibu zao YouTube ni Lazima wauweka ‘Private’ wakati wakiendelea na taratibu za kujiridhisha juu ya madai hayo na kama uongozi wa Harmonize tayari tumesha waelekeza wataalam wetu wa kisheria kufuatilia jambo hili kwa kina.