VIDEO: Wizkid, Tiwa Savage walizungumzia tamasha la Wasafi, Diamond awapa tuzo

Muktasari:

Wasanii wa Nigeria waimwagia sifa Tanzania, wampongeza Diamond kwa kufanya tamasha lililowaunganisha wasanii wa Afrika.

Dar es Salaam. Mwanamuziki wa nchini Nigeria, Wizkid ameeleza kuwa alichokifanya Diamond kupitia tamasha la Wasafi ni mfano wa kuigwa kwa wasanii wa Afrika.

Wizkid ameyasema hayo leo Jumatatu Novemba 11, 2019 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam ukiwahusisha wasanii walioshiriki tamasha hilo.

Amesema tamasha hilo ni mfano mwingine wa kuonyesha wasanii wa Afrika ni kitu kimoja na wanashirikiana katika kazi.

“Sijaja kwa sababu naipenda Diamond au naipenda Tanzania bali nimekuja kwa sababu ni tamasha ambalo limewaunganisha wasanii wa Afrika.”

“Hii ni hatua kubwa kwa wasanii kushirikiana na kuungana mkono na inavutia kuona wasanii wanashirikiana. Endeleeni kuunga mkono muziki wa Afrika ili ufike mbali zaidi,” amesema

Kwa upande wake, Tiwa Savage ameisifia Tanzania kuwa ni nchi yenye watu wakarimu na upendo mkubwa kwa wasanii wao.

Amesema ni wakati wa wasanii wa Afrika kushirikiana na kuungana mkono na dunia ijue kuwa Waafrika wako pamoja.

“Nikupongeze Diamond na timu yako kwa kufanya shoo ambayo inaenda kusaidia matibabu ya watoto, ambayo imetuma nafasi ya sisi pia kushiriki,” amesema

Katika mkutano huo Diamond kupitia Wasafi Media amewakabidhi tuzo za shukrani wasanii hao akieleza kuwashukuru kwa namna ambavyo wamejitoa kushiriki kwenye tamasha hilo.

Tamasha hilo lilifanyika Jumamosi iliyopita ya Novemba 9, 2019 jijini Dar es Salaam ambapo asilimia 80 ya mapato yatakwenda kugharamikia matibabu ya moyo kwa watoto waliopo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).