Zamaradi Mketema aja na filamu ya Sh200 milioni

Muktasari:

  • Mtangazaji Zamaradi Mketema ametengeneza filamu iliyogharimu zaidi ya Sh200 milioni huku akiahidi kuleta mabadiliko katika soko la filamu nchini Tanzania

Dar es Salaam. Mtangazaji maarufu nchini Tanzania, Zamaradi Mketema amekuja na filamu iliyomgharimu Sh200 milioni katika kuitengeneza huku akieleza kuwa filamu hiyo imekuja kuleta mapinduzi katika sekta ya filamu.

Filamu hiyo inayoitwa 'Cop's Enemy' aliyoanza kuitengenezwa tangu mwaka 2016 na prodyuza John K, imechezwa katika nchi tatu ikiwemo Tanzania, Australia na India.

Wakati wasanii walioshirikishwa wamo Wema Sepetu, Stanlenley Msungu na Aunt Ezekiel kutoka Bongo, Van Vicker wa Ghana na wengine kutoka Nigeria, India na Australia.

Zamaradi ambaye aliwahi kuongoza filamu ya Kigodoro Kantangaze na Nzowa, akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Februari 4, 2019 amesema utengenezaji wa filamu hiyo ya gharama umelenga kuleta mapinduzi katika tasnia ya filamu hapa nchini ambayo imeonekana kushuka.

Amesema kutokana na hilo hakuhofia gharama watakazotumia kwani shida ilikuwa wafanye kitu kizuri kitakachorudisha heshima ya filamu nchini Tanzania.

Kwa upande wa waongozaji yupo Neema Ndempayo na John K kutoka nchini Australia ambaye pia ni mmoja wa wahusika katika filamu hiyo.