Ubingwa Ufaransa waua mashabiki wawili

Muktasari:

  • Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki hao waliojitokeza kwa wingi Champs-Elysees kusherekea ubingwa huo.

Paris, Ufaransa. Mashabiki wawili wamekufa nchini Ufaransa wakati wakishangilia timu yao ya taifa kuifunga Croatia na kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia jijini Moscow.

Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki hao waliojitokeza kwa wingi Champs-Elysees kusherekea ubingwa huo. 

Mashabiki hao walirusha mabomu yaliyotoa moshi wa bendera ya timu ya taifa ikiwa na rangi ya blue, nyeupe na nyekundu wakati polisi walitumia maji kupambana nao.

Watu walikimbia katika vibanda vya kuuzia magazeti pamoja na vituo vya basi wakipeperusha bendera huku wimbo wa taifa wa Marseillaise ukisikika mitaani pamoja na honi za magari kutoka kwa mashabiki hao.

Lakini mashabiki hao waliokuwa wakishangilia walipofika mbele ya maduka makubwa walivunja vioo kabla ya Polisi kuingilia kati kuzuia uhalifu huo.

Katika mji wa Alpine, Annecy, shabiki mmoja mwenye miaka 50, alidondoka kwenye mfereji na kuvunjika shingo na kufariki akishangilai ushindi wa mabao 4-2. Pia, karibu na mji wa Saint-Felix kilitokea kifo kingine kwa kijana mwenye miaka 30 kugongwa na gari akisherekea ushindi.

Vurugu kubwa ilikuwa katika jiji la Lyon, ambako mamia ya vijana walishambulia magari na kuwasha matairi moto mitaani.

Picha moja ya video ilionyesha duka la nguo la Lacoste likiwa limevamiwa na wezi waliokuwa wamevalia jezi za timu ya taifa ya Ufaransa.