#WC2018: Mabao ya Varane, Griezmann yaipeleka Ufaransa nusu fainali

Friday July 6 2018

 

Nizhny, Russia. Mabao mawili yaliyowekwa kimiani na Rafael Varane na Antoine Griezmann yalitosha kuwazima Uruguay na kuihakikishia Ufaransa nafasi katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Dunia 2018.

Varane anayekipiga katika klabu ya Real Madrid, alipiga kichwa safi kunako dakika ya 40, akiunganisha krosi ya Antoine Griezmann ambaye alikuwa mwiba mchungu kwa Uruguay, katika mchezo huo wa kwanza wa robo fainali, uliomalizika muda mfupi uliopita katika uwanja wa Nizhny Novgorod.

Kipindi cha kwanza kikamalizika Ufaransa wakiwa kifua mbele ya bao 1-0 dhidi ya Uruguay iliyokuwa ikimkosa straika wake matata, Edinson Cavani. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Uruguay wakionekana kukubali matokeo mapema tu.

Wakijivunia umiliki wa mpira kwa asilimia 58 dhidi ya 42, Les Blues, walipata bao lao la pili katika dakika ya 61, mfungaji akiwa ni Antoine Griezmann. Utamu bao hili ni kwamba, Kipa wa Uruguay alijikuta akishindwa kuhimili kishindo cha shuti la Griezmann, akirudia kosa lililofanywa na kipa wa Liverpool, Loris Karius katika mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya, unakumbuka?

Ushindi wa mabao mawili walioupata kwenye mchezo unawapa tiketi ya kumsubiri mshindi wa mechi ya robo fainali ya pili, utakaopigwa baadae kati ya Brazil na Belgium. Ushindi wa kikosi cha Didier Deschamps, pia unamaanisha kuwa Ufaransa wamefuzu kucheza nusu fainali ya Kombe la Dunia, kwa mara ya sita mfululizo.