#WC2018: Messi ndiye mwenye fainali zake huko Russia

Muktasari:

Ronaldo na Mo Salah vita yao ni moja tu, kujisogezea Ballon d’Or karibu yao zaidi. Kwa kile walichokifanya kwenye klabu zao huko Real Madrid na Liverpool kwa msimu uliopita, wanahitaji kutamba kidogo tu kwenye Kombe la Dunia kujihalalishia nafasi ya kuibeba tuzo hiyo ya Ballon d’Or.

CRISTIANO Ronaldo na Mohamed Salah. Eden Hazard na Neymar. Kisha kuna Lionel Messi katika vita ya yeye mwenyewe.

Ronaldo na Mo Salah vita yao ni moja tu, kujisogezea Ballon d’Or karibu yao zaidi. Kwa kile walichokifanya kwenye klabu zao huko Real Madrid na Liverpool kwa msimu uliopita, wanahitaji kutamba kidogo tu kwenye Kombe la Dunia kujihalalishia nafasi ya kuibeba tuzo hiyo ya Ballon d’Or.

Neymar na Hazard vita yao ipo kwenye tiketi ya kutua Bernabeu. Wanafahamu wazi, atakayetamba zaidi huko Russia, basi Los Blancos hawawezi kumuacha.

Sawa, pengine Neymar asitazamwe zaidi kwa michuano hiyo na Los Blancos, lakini kwa upande wa Hazard itakuwa hivyo kwa sababu hakuwa na wakati mzuri sana na Chelsea yake kwa msimu uliopita.

Hata hivyo, ukiacha vita ya hivyo, mastaa hao wote wanabeba matumaini makubwa ya mataifa yao kuhakikisha wanaleta furaha nyumbani.

Ronaldo kwa Wareno, Salah kwa Wamisri, wakati Hazard ni Wabelgiji na Neymar ni Wabrazili, ambao miaka minne iliyopita walimwaga chozi walipochapwa Bao Saba na Ujerumani. Wanahitaji faraja ya kufanya vyema huko Russia. Kisha anakuja Messi sasa.

Kama Argentina itashinda ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka huu, Messi atakuwa amefunga mjadala. Hapo itakuwa rasmi kwamba ndiye mwanasoka bora zaidi kuwahi kutokea kwenye soka. Hii ndiyo maana nasema Messi yupo kwenye vita dhidi yake mwenyewe.

Amewabeba Argentina kufika kwenye fainali hizo za Russia, hivyo anatazamwa kuwabeba tena kuwapa ubingwa baada ya kushindwa kufanya hivyo miaka minne iliyopita. Argentina ilifika fainali huko Brazil, ikapofungwa na Ujerumani bao 1-0.

Lakini, halikuwa gundu la kwanza kwa Messi kupoteza fainali kwenye kikosi chake cha Argentina, akichapwa mara mbili mfululizo kwenye fainali ya Copa America, tena dhidi ya timu moja, Chile ya Alexis Sanchez na mwenzake Arturo Vidal.

Huu ni mwaka wa Messi. Kwa sababu ni wazi kabisa hizi zitakuwa fainali zake za mwisho za Kombe la Dunia akiwa kwenye ubora wake huu tunaomshuhudia kuwa nao. Pengine Hazard, Salah na Neymar bado wanamatumaini ya fainali nyingine zile zitakafanyika Qatar, lakini kwa Messi hii ni risasi yake ya mwisho.

Hakuna ubishi, kubeba ubingwa wa dunia kutamfanya Messi kutambulika kama mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea duniani.

Amebeba makombe yote anayopaswa kubeba kama mchezaji, imebaki taji la dunia tu kumfanya kuingia kwenye kundi la magwiji kama Pele na Diego Maradona.

 Mpinzani wake, Ronaldo ana kitu cha kujivunia, hata akiondoka patumu huko Russia kuna sehemu inayomfanya aweke jina lake kwenye rekodi tamu zaidi.

Kwa sababu ameshinda kila alichokishinda Messi na kumwongezea sifa zaidi ni kubeba ubingwa wa Ulaya. Sawa, Messi na medali ya Olimpiki, lakini hilo haiwezi kufua dafu kwenye medali ya ubingwa wa Ulaya aliyobeba Ronaldo akiwa na Ureno miaka miwili iliyopita.

Kwa maana hiyo, fainali hizo za Russia unaweza kusema zinamhusu zaidi Messi kuliko mchezaji mwingine yeyote yule.

Kitu kizuri uwepo wake ndio unaofanya Argentina kuwa moja ya taifa linalopewa nafasi kubwa ya kubeba ubingwa, lakini kubeba ubingwa wa michuano hiyo unahitaji kuzikabili timu ngumu kama Brazil, Ujerumani, Hispania, Ufaransa, Ubelgiji na kisha uwe umeibuka na ushindi. Huo ndio ugumu wa kubeba ubingwa wa michuano kama hiyo ya Kombe la Dunia, unapaswa kuzishinda timu ngumu.

Kazi ngumu kwa Messi inaanzia kwenye kundi lake tu. Kuzikabili Iceland, Croatia na Nigeria si kitu chepesi. Akipita hapo, pengine itamfungulia njia zaidi ya kutambua kwamba hapo atakuwa na hatua chache tu za kwenda mbele kabla ya kufikia kilele cha mafanikio anayoyafukuzia.

Ni mwezi mmoja mgumu kwenye mapito mengi na hakika anahitaji msaada muhimu kutoka kwa watu kama Paulo Dybala, Sergio Aguero na Angel Di Maria kukamilisha ndoto ambazo zitamfanya Lionel Messi kuwa mwanasoka bora kabisa kwenye safari hii inayoitwa dunia. Kazi ni kwake!