#WC2018: Pogba: Watu wanachonga sana juu yangu

Muktasari:

  • Kiungo huyo ni mmoja wa wachezaji ghali zaidi wanaocheza Kombe la Dunia

Moscow, Russia. Kiungo wa Ufaransa, Paul Pogba ameibuka na kudai kuwa, miongoni mwa wanasoka walioko nchini Russia, katika mashindano ya Kombe la Dunia, ndiye anayeongoza kwa kusemwa duniani. Hii kali!

Pogba alikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa 2-1 walioupata dhidi ya Australia, alisababisha penalti iliyofungwa na Antoinne Griezmanne kabla ya kushuhudia shuti lake likimbabatiza beki wa Australia na kuzaa bao la pili na la ushindi.

Kiungo huyo wa Manchester United, mwenye umri wa miaka 25, alikuwa na kiwango mbovu katika klabu yake na taifa lake, msimu wa 2017-18, ambapo mara nyingi alijikuta akishutumiwa na mashabiki kote ulimwengu, lakini anasema hilo halimsumbui.

"Inaonyesha mimi sipaswi kufanya makosa, kila siku naandamwa mimi tu, inachekesha sana. Kutokea kuwa sajili ghali zaidi duniani hadi mchezaji anayeandamwa zaidi duniani sio jambo jema, ila sijali", alisema Pogba.

Baada ya kuvuna ushindi katika mchezo wao wa kwanza, timu ya taifa ya Ufaransa ‘Les Blues’, inatarajia kuingia dimbani Alhamisi kumenyana na Peru katika mchezo wao wa pili wa makundi.