#WC2018: Southgate ameanza kuchonga, ana kiburi kinoma

Wednesday July 4 2018

 

By Fadhili Athumani

Moscow, Russia. Ushindi mtamu bwana asikwambie mtu. Jana nani alimuona Kocha wa England, Gareth Southgate alivyokuwa kalowa baada ya lile bao la Yerry Mina? Alikuwa mpole balaa. Walivyoshinda kwa matuta je? Unaambiwa jamaa si ameanza kuchonga, ana kiburi kinoma.

Baada ya kuivusha England kwenda hatua ya robo fainali, tena kwa matuta, Kocha wa England eti naye ameanz kuvimba. Ndio, Gareth Southgate alinukuliwa akisema wao hawaamini katika historia, kazi yao ni kutembeza kichapo tu! Ushindi bwana?

Ni hivi, kitendo cha kuichapa Colombia kwa mikwaju ya penalti iliyomshuhudia kipa wao, Pickford akiokoa shuti la Carlos Bacca, baada ya shuti la Matues Uribe kugonga besela, huku Eric Dier akikwamisha mkwaju wa mwisho wavuni na kuwapa ushindi wa mabao 4-3, England walifanikiwa kuondoa gundu la miaka mingi kwenye michuano hii.

Rekodi zinaonesha kwamba, tangu mwaka 1996, walipoing'oa Ureno kwa mikwaju ya penalti katika michuano ya kombe la Euro, Three Lions haikuwahi kushinda mchezo wowote ule kwa mikwaju ya penalti, unashangaa? Ndio, England walikaa miaka 22 wakichezea vichapo tu walipofika hatua hiyo, ila jana walivuka mwanangu.

Kutokana na hilo, Gareth Southgate amegeuka Haji Manara wa Ulaya, anachonga kinoma. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mchezo, kocha huyo, ambaye alikuwa sehemu ya kikosi kilichoitandika Colombia 2-0 huko France, miaka 20 iliyopita, alisema wao hawatambui mambo ya historia.

Southgate, ambaye ndiye aliyekosa mkwaju wa penalti, miaka 22 iliyopita katika mchezo wa kombe la Euro 1966 dhidi ya Ujerumani, alisema katika kikosi chake ana vijana wadogo wenye uwezo mkubwa kwa hiyo kuwabebesha mizigo ya historia ni kuwaonea na jana wamethibitisha hilo.

"Kumbukumbu hiyo itaendelea kuwa sehemu ya maisha yangu. Ni ngumu kusahau. Hata hivyo sio haki kuwabebesha vijana hawa mizigo ya historia, sisi hatutambui hayo mambo, kwa sasa tunalengo moja tu, kutembeza kichapo kwa kila anayekatiza mbele yetu. Tunawaza mchezo wa robo fainali," alisema Southgate na kuongeza

"Katika maisha ni kosa kuruhusu hisia za watu historia au matamanio ya watu yatumike kuamua kesho yako, ukifanya hivyo umekwisha. Akili na nguvu zetu tunazielekeza kwa Sweden na sio mambo ya zamani. Tumethibitisha kuwa historia haina nafasi kwa kuifunga Colombia."