#WC2018: Yametimia! Ufaransa mabingwa kombe la dunia

Sunday July 15 2018

 

By Fadhili Athumani

Moscow, Russia. Hatimaye Ufaransa wametawazwa mabingwa wapya wa Kombe la Dunia, baada ya kuibugiza Croatia mabao 4-2 katika mchezo mkali wa fainali iliyomalizika muda mfupi uliopita katika uwanja wa Luzhniki mbele ya mashabiki 81,000.

Les Blues ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao, katika dakika ya 18, baada ya Mario Mandzukic kujifunga katika juhudi za kuokoa mpira, uliochongwa na straika wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann. Dakika 10 baadaye Croatia wakasawazisha kupitia kwa Ivan Perisic.

Mchezo huo ulilazimika kusimama kwa dakika tatu, kunako dakika ya 34 kwa ajili ya kupisha teknolojia ya VAR, kutatua utata ulioibuka baada ya Ivan Perisic kuunawa mpira ndani ya boksi katika juhudi za kuokoa mpira wa kona.

 

Mwamuzi wa mechi Nestor Pitana, kwa msaada wa VAR, akaamua kuwazawadia Ufaransa penalti na Antoine Griezmann akaukwamisha wavuni. Dakika tatu za nyongeza kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza kilishuhudia Croatia wakiandama lango la Ufaransa bila mafanikio kwa lengo la kusawazisha. Hadi wanaenda mapumziko, matokeo ni 2-1.

Kipindi cha pili, Croatia waliingia wakiwa na ari ya kusawazisha lakini wakajikuta wakipigwa bao la tatu, kunako dakika ya 59, mfungaji akiwa ni kiungo wa Manchester United, Paul Pogba, dakika sita baadaye, Winga wa Paris saint-Germain anayewindwa na Real Madrid, Julian Mbappe akaweka bao nne kambani.

Wakiwa na nguvu kama kawaida yao, 'watoto wa mama' Croatia waliendelea kushambulia lango la Ufaransa ambapo uzembe wa kipa na nahodha wao, Hugo Lloris, ulimpa Mario Mandzukic nafasi ya kurekebisha makosa na kuifungia timu yake bao la pili.