#WC2018: Gazza ampa mbinu kocha England

Wednesday July 11 2018

 

Moscow, Russia. Zikiwa zimebaki saa chache kabla ya England kuvaana na Croatia, kiungo nguli wa zamani Paul Gascoigne ‘Gazza’ amempa mbinu za ushindi Gareth Southgate.

England na Croatia zinatarajiwa kupepetana katika mchezo wa nusu fainali ya pili kwenye Uwanja wa Luzhniki, Russia.

Gazza aliwahi kucheza na Southgate kikosi cha England kwenye Fainali za Kombe la Ulaya mwaka 1996 ambapo walifungwa na Ujerumani kwa penalti katika mchezo wa nusu fainali.

Katika mchezo huo, Gazza alilimwa kadi ya njano ambapo alimwaga chozi uwanjani kwa kuwa aliamini angekosa mchezo wa fainali.

Mbali na kucheza pamoja, Gazza na Southgate ni marafiki wa karibu ingawa kiungo huyo ‘amepotea’ katika ramani ya soka kutokana na matumizi makubwa ya pombe.

Nyota huyo wa zamani wa Newcastle United na Tottenham Hotspurs, alimtaka Southgate kutohofia mchezo huo.

“Gareth hongera sana rafiki yangu, unafanya kazi nzuri. Jikite katika kile unachokiamini, niko nyuma yako,” alisema Gazza, mmoja wa viungo bora waliowahi kutokea duniani.

Gazza alisema hafahamu kocha huyo anazungumza nini na wachezaji, lakini na amini anafanya kazi nzuri na England itapata mafanikio.

Nguli huyo mwenye miaka 51, amekwenda Russia kushuhudia mchezo huo ambao England inawania taji hilo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1966 ilipotwaa Kombe la Dunia kwenye Uwanja wa Wembley.

“Nadhani wachezaji wote wamecheza kwa kiwango bora, lakini wanakutana na timu ngumu hivyo kila mmoja anapaswa kuwa nahodha. Wanatakiwa kucheza kwa kasi kuwafurahisha mashabiki ambao watakuwa nyuma yao wakiwaimbia,” alisema Gazza.