#WC2018: Kilichoipeleka nusu fainali England hiki

Monday July 9 2018

 

Moscow, Russia. Kocha wa England, Gareth Southgate amesema mafanikio ya timu hiyo katika Fainali za Kombe la Dunia, yametokana na ujasiri wa wachezaji.

Kauli ya Southgate imekuja muda mfupi baada ya England kufuzu nusu fainali kwa kuichapa Sweden mabao 2-0 juzi jioni.

Kocha huyo alisema aliwajenga kisaikolojia wachezaji miezi 18 kabla ya kuanza fainali hizo kwa kuwaambia wanaweza kupata mafanikio nchini Russia.

Pia alisema msingi mzuri uliojengwa na mtangulizi wake Roy Hodgson umechangia kupata kikosi bora katika fainali hizo.

“Niliwaambia mafanikio makubwa mtakayopata katika timu ya Taifa ni tofauti na ngazi ya klabu. Labda kwa sababu niliwaeleza ukweli kila wakati,” alisema Southgate.

Alisema muda mfupi baada ya kukata tiketi kushiriki fainali hizo, aliweka bayana kwa vyombo vya habari mkakati wa kuivusha England.

“Timu ilizungukwa na mashabiki wote wa England na hakuna maswali nilifungua milango kwa vyombo vya habari kuandika habari zetu, ilitusaidia,” alisema Southgate.

Pia alisema msingi mzuri ulioachwa na kocha wa zamani wa timu hiyo Hodgson, ulikuwa na manufaa makubwa ingawa mara kwa mara alikuwa akimkosoa.

“Roy alikuwa akinikosoa mara kwa mara, lakini anastahili kupongezwa kwa kazi nzuri ya kuweka msingi imara kwa wachezaji chipukizi. Kama nisingekuwa na wachezaji wazoefu tusingefika hapa,” alisema kocha huyo.

Southgate alisema wachezaji Dele Alli, Eric Dier, Harry Kane na Kyle Walker ni matunda ya bosi huyo wa zamani wa Liverpool.