#WC2018: Kocha Ujerumani aweweseka

Muktasari:

Ujerumani ni bingwa mtetezi wa Kombe la Dunia

Moscow, Russia. Bao lililofungwa na mshambuliaji wa Mexico, Hirving Lozano ‘Chucky’ limemuweka Kocha Joackim Low wa Ujerumani katika wakati mgumu.

Akizungumzia kipigo hicho cha kustusha Low aliwaomba radhi mashabiki wa Ujerumani ana akasema limewaamsha na kuwataka wasiwe na wasiwasi akiwaahidi kushinda mechi mbili zilizobakia ili waweze kutinga raundi ya pili.

“Tunaomba radhi kwa kuputeza mchezo huu, tunaomba hili liongeze mshikamno wetu wajerumani wote, tunaahidi kufanya vema katika mechi zijazo, mchezo wetu na  ya Sweden wa Juni 23 na ule wa mwisho wa makundi dhidi ya Korea Kusini, Juni 27, tunaomba waendelee kutunuunga mkono,” alisema Low.

Aliwasihi mashabiki wao kutomtupia lawama kipa Manuel Neuer akisema bao alilofungwa halikutokana na uzembe bali ni makosa ya timu nzima.

Low aliyedumu katika nafasi hiyo kwa kipindi kirefu, alisema hakuna aliyetarajia kuwa wangepoteza mchezo huo licha ya kufungwa katika dakika ya 35.

Alikiri kuwa kasi ya washambuliaji wa hasa Javier Hernandez ‘Chicharito’, ilikuwa sababu ya wao kupoteza mchezo kwani tangu alipotia pasi iliyoza bao ilibidi wamchunge asilete madhara zaidi.

Kipigo hicho kimeibua mengi kiasi kwamba baadhi ya mashabiki wameanza kumnyooshea vidole vya lawama Kocha Low  kuhusiana na uteuzi wake wa wachezaji alioenda nao Russia wakidai aliangalia zaidi uzoefu na kuacha damu change ambao wangehimili mbio za Mexico.