#WC2018: FAINALI: Kumekuchaa!! Kipindi cha kwanza Ufaransa 2-1 Croatia

Sunday July 15 2018

 

Moscow, Russia. Uwanja wa Luzhniki unawaka moto, ni ubabe tu Ufaransa wakienda katika vyumba vya kubadilishia nguo wakiwa kifua mbele, kwa mabao 2-1, dhidi ya Croatia katika mchezo mkali wa Fainali unaoendelea muda huu, huko Russia.

Ufaransa walikuwa wa kwanza kupata bao, katika dakika ya 18, baada ya Mario Mandzukic kujifunga katika juhudi za kuokoa mpira wa freekick, uliochongwa na straika wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann. Dakika 10 baadae Croatia wakasawazisha kupitia kwa Ivan Perisic.

Mchezo huo ulilazimika kusimama kwa dakika tatu, kunako dakika ya 34 kwa ajili ya kutafuta msaada wa VAR, baada ya kuibuka utata kuhusu kama ni penalti au sio kufuatia mpira wa kona kumgusa Ivan Perisic mkononi. Baada ya kujihakikisha, Mwamuzi wa mechi Nestor Pitana, kwa msaada wa VAR aliwapatia Les Blues Penalti na Antoine Griezmann akaukwamisha wavuni.

 

 

Dakika tatu za nyongeza kabla ya kumalizika kwa kioindi cha kwanza kilishuhudia Croatia wakiandama lango la Ufaransa bila mafanikio kwa lengo la kusawazisha. Hadi wanaenda mapumziko, matokeo ni 2-1.