Mbappe ang’aka kufananishwa na Pele

Monday July 16 2018

 

Paris, Ufaransa. Mashindano ya Kombe la Dunia iliyomalizika jana na kuishuhudia Ufaransa likitawazwa kuwa bingwa wa dunia kwa mara ya pili, imeondoka na kumuacha winga wa PSG akijiachia katika meza moja na mkongwe wa soka, Mbrazil Pele.

Ndio, taka usitake Mbappe siyo wa sayari hii. Baada ya kuingia uwanjani na jezi ya Les Blues kwenye mashindano ya mwaka huu, Mbappe hakuisaidia Ufaransa kutwaa ubingwa wa Dunia tu, bali pia aliamua kuvunjilia rekodi nne tofauti.

Rekodi ya kwanza ilikuwa ni ya Mfaransa mwenzake,  David Trezeguet, iliyodumu kwa miaka 20, huku tatu zilizosalia zikiwa ni za Pele, zilizodumu kwa miaka 60! Unashangaa? Habari ndio hiyo mwanangu.

Juni 21, katika mchezo wa pili wa kundi C, Ufaransa walikutana na Peru, wakashinda 1-0, lililowekwa kambani kunako dakika ya 34, mfungaji akiwa ni Kylian Mbappe. Bao hili, lilimfanya Mbappe avunje rekodi ya mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kufunga bao katika Kombe la Dunia.

David Trezeguet aliweka rekodi hiyo mwaka 1998, akiwa na umri wa miaka 20. Mbappe alifunga bao lake akiwa na miaka 19 na siku 154.

Baada ya hapo, katika mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Argentina, Mbappe alitupia mara mbili na kuvunja rekodi ya Pele, aliyoiweka mwaka 1958.

Rekodi hiyo, ni ya mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kufunga mabao mawili katika mechi moja ya Kombe la Dunia. Kama hiyo haitoshi, katika ushindi wa jana wa 4-2 walioupata dhidi ya Croatia Mbappe alifunga bao la nne.

Bao hilo lilivunja rekodi ya Pele ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kufunga kwenye mechi ya fainali ya Kombe la dunia.

Maajabu ya Mbappe hayakuishia hapo, kitendo cha Ufaransa kubeba ndoo kilimaanisha kuwa amevunja rekodi ya mchezaji kinda aliyesinda Kombe la Dunia, iliyowekwa na Pele.

Baada ya kufanya hayo aliyoyafanya, watu si wameanza kumfananisha na mfalme soka (Pele). Eti kwa sababu ameweza kutafuna mfupa uliowashinda mastaa wengi kama Zinedine Zidane, Ronaldo de Lima, Neymar, Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, eti watu wanasema amefanana na Pele. Umesikia jibu la Mbappe lakini?

Akizungumza muda mfupi baada ya kutwaa ubingwa wa Dunia, winga huyo wa Paris Saint-Germain, amecharuka kinoma, akiwataka watu waache kumlinganisha na Pele, huku akisisitiza kuwa yeye anajenga ufalme wake mwenyewe.

"Hakuna wa kufanana na Pele, yule walikuwa mchawi wa soka, nafarijika sana kufananishwa naye, lakini nadhani ni vyema watu wakaelewa kuwa Mbappe anajenga ufalme wake, Mbappe anajitengezea njia yake mwenyewe. Hatufanani hata kidogo," alisema Mbappe.