#WC2018: Neymar abadili gia, amgeukia Mungu

Muktasari:

  • Neymar alidokeza kitendo cha Brazil kuondolewa kwenye Fainali za Kombe la Dunia, kimempa maumivu makali ambayo yanaweza kutishia maendeleo yake ya soka.

Moscow, Russia. Baada ya kuondolewa katika Fainali za Kombe la Dunia, mshambuliaji nyota wa Brazil, amesema ni Mungu pekee anayeweza kumpa nguvu ya kurejea uwanjani akiwa kwenye kiwango bora.

Neymar alidokeza kitendo cha Brazil kuondolewa kwenye Fainali za Kombe la Dunia, kimempa maumivu makali ambayo yanaweza kutishia maendeleo yake ya soka.

“Nimeumia sana, nilikuwa na matarajio makubwa Brazil itapata mafanikio katika fainali hizi, lakini imekuwa tofauti.

Nina wakati mgumu kurejesha kiwango changu uwanjani, inaweza kuchukua muda mrefu, lakini naamini Mungu pekee ndiye atakayenipa nguvu,” alisema Neymar.

Mchezaji huyo wa Paris Saint Germain (PSG), alisema walikwenda Russia kushiriki fainali hizo akiwa na matumaini ya Brazil kuweka historia.

Ndoto ya Neymar ilizimwa na Ubelgiji, baada ya kucharazwa mabao 2-1 katika mchezo wa robo fainali.

Neymar aliyefunga mabao mawili katika fainali hizo, alisema ni jambo la kujivunia kuwa sehemu ya timu ya Taifa, lakini haiondoi ukweli kuwa ameumia kwa kiasi kikubwa baada ya Ubelgiji kuzima ndoto zao.

Timu hiyo jana ilirejea Brazil na mshambuliaji huyo anatarajiwa kwenda Paris, Ufaransa kujiunga na kambi ya PSG kwa maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu.

Brazil ni miongoni mwa timu zilizokuwa zikipewa nafasi ya kutwaa ubingwa katika fainali hizo kabla ya Ijumaa usiku kung’olewa kwenye Uwanja wa Kazan. Brazil imetwaa ubingwa mara tano.