#WC2018: Ronaldo aweka rekodi mpya Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo wa Ureno anashikiria rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi Ligi ya Mabingwa Ulaya

Moscow, Russia. Cristiano Ronaldo amekuwa mchezaji wa kwanza duniani kufunga mabao katika mashindano nane makubwa baada ya kuifunga goli tatu Hispania katika sare 3-3.

Bao la penalti katika dakika ya tatu katika Kombe la Dunia kati ya Ureno na Hispania limefanya Ronaldo kuwa mchezaji wa kwanza kufunga katika mashindano nane makubwa duniani. 

Mashindano makubwa yanayotajwa hapa ni Kombe la Dunia, Kombe la Mataifa ya Ulaya au Copa Amerika. 

Tangu alipoanza kuichezea Ureno katika mashindano makubwa Euro 2004, Ronaldo amekuwa akifunga japo bao mmoja katika kila mashindano aliyoshiriki na timu ya taifa.

Mshambuliaji huyo wa Ureno anakuwa mchezaji wan ne kufunga katika mashindano manne ya Kombe la Dunia kuanzia 2006, 2010, 2014 na 2018 – baada ya Pele, Uwe Seeler na Miroslav Klose. Mshambuliaji wa Australia,Tim Cahill anaweza kuwa wa tano kama atafunga katika fainali hizi za Russia. 

Ronaldo alimaliza mchezo huo kwa kufunga mabao matatu ‘hat-trick’, baada ya ile penalti ilifuatiwa na lile bao la dakika 44, lililosababishwa na uzembe wa kipa wa Hispania, David De Gea. 

Pia, Ronaldo alitimisha kwa kufunga bao la tatu kwa mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni na kuihakikishia Ureno pointi moja muhimu katika sare 3-3 dhidi ya Hispania.

Ronaldo kama ataendelea na kasi hiyo ya kufunga mabao katika mechi mbili za kundi hilo dhidi ya Morocco na Iran anaweza kuwa mfungaji bora wa mashindano haya.