#WC2018: Ronaldo tumemuona, leo zamu ya Messi, Griezmann

Muktasari:

  • Ufaransa vs Australia, Argentina vs Iceland, wakati kesho Ujerumani vs Mexico, Brazil vs Uswisi

Moscow, Russia. Ingawa mechi za ufunguzi wa fainali za 21 za Kombe la Dunia ilipigwa juzi wenyeji na Russia wakaichapa Saudi Arabai mabao 5-0, mashabiki wa soka walihesabu kuwa uhondo wa mechi hizo ulianza jana.

Mechi baina ya Misri na Uruguay iliyomalizika kwa mabingwa 1930 kushinda bao 1-0 mjini Ekaterinburg huku Morocco ikichapwa 1-0 na Iran zilipewa umuhimu zaidi na mashabiki kuliko ile ya ufunguzi.

Kama hiyo haitoshi mchezo baina ya Ureno inayoongozwa na Cristiano Ronaldo aliyefunga mabao matatu dhidi ya Hispania katika sare 3-3 ndio ulioonekana kukusanya mashabiki wengi zaidi kwenye luninga hapo jana.

Baada ya mechi hizo kumalizika kimbembe kinatarajiwa kuwa leo pale Argentina nchi inayoongoza kwa kusheheni masupa staa wakiongozwa na Lionel Messi watakaposhuka uwanja mjini Bronnitsy, kukipiga na Iceland katika mchezo wa kundi D.

Wengi wanaziona fainali za mwaka huu kama za mwisho kwa Messi mwenye miaka 31, pamoja na nahodha wa Ureno, Cristiano Ronaldo.

Ingawa Iceland, ilifika hatua ya robo fainali katika fainali za Euro 2017, nchini Ufaransa na tambo za Kocha wake Heimar Hallgrimsson, haitarajiwi kufurukuta mbele ya Argentina.

Kocha wa Argentina, Jorge Burruchaga, aliuambia mtandao wa FIFA kuwa anaamini Argentina haitembelei nyota ya Messi bali inao wachezaji wengi wenye uwezo na uzoefu.

Alisema wanajivunia ukuta wao unaoongozwa na walinzi wanaocheza katika Ligi kuu England, Nicolas Otamendi wa Manchester City, Marcos Rojo anayeitumikia Manchester United na mlinzi mkongwe Javier Mascherano.

Alisema kupoteza fainali iliyopita kwa Ujerumani katika muda wa ziada na kupoteza mechi mbili za fainali ya Copa America kunawapa morari zaidi.

Fainali hizi pia zinaonekana kuwa za mwisho pia kwa mshambuliaji Sergio Aguero aliyeifungia mabao 37 kwa mechi  85, anayemfahamu vizuri beki tegemeo wa Iceland Gylfi Sigurdsson wanayecheza pamoja Man City.

Katika mchezo wa leo kwenye dimba la Spartak Stadium mjini Moscow Iceland watamtegemea kiungo na nahodha wao Aron Gunnarsson.

Ufaransa vs Australia

Mbali ya mchezo huo, leo pia kutakua na mtanange kati ya  mabingwa wa Kombe la Dunia mwaka 1998 Ufaransa dhidi ya Australia, mchezo wa kundi C utakaopigwa mjini Kazan.

Ufaransa ndiyo inayopewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo kutokana na kusheheni vipaji kwenye kikosi chake wakiwemo Paul Pogba, Ousmane Dembele, Kylian Mbappe, Nabil Fekir, Olivier Giroud na Antoine Griezmann.

Vijana hao wa Kocha Didier Deschamps maarufu kama ‘Les Bleus’ wanajivunia sana sehemu yao ya kiungo inayoongozwa na Blaise Matuidi, Steven Nzonzi na N'Golo Kanté, ambao wapo katika kiwango bora sana kwa sasa.

Wachezaji wa Ufaransa wamemuahidi shujaa wa Taifa hilo Zinedine Zidane kwamba watahakikisha wanafuata nyayo zake alipoipa Ufaransa ubingwa pekee wa Dunia mwaka 1998.

Mechi nyingine zitakazopigwa leo ni ile itakayowahusisha wawakilishi wengine wa Afrika, Nigeria ‘Super Eagles’ mchezo wa kundi D, watakapokipiga dhidi ya Croatia mjini Kaliningrad na Peru dhidi ya Denmark mchezo wa kundi C, mchezo utakaopigwa mjini Saransk.

Ratiba

Ufaransa v Australia ( Saa 7:00 mchana)

Argentina v Iceland ( Saa 10:00 Jioni)

Peru v Denmark (Saa 1:00 Usiku)

Croatia v Nigeria (Saa 4:00 Usiku)