#WC2018: Samuel Umtiti: Mkimbizi aliyeing’oa Ubelgiji St. Petersburg

Wednesday July 11 2018

 

By FADHILI ATHUMANI

USIKU wa jana Jumanne usiku, Julai 10, mwaka huu, Dimba la Saint Petersburg, ukiwa umejaa watazamaji 67,000, wengi wao wakiwa ni watu weusi wenye asili ya bara la Afrika, nusu yao wakiwa ni Wazungu kutoka Ubelgiji na mataifa mengine ya Ulaya, walishuhudia kifo cha Ubelgiji katika mikono ya 'Mwafrika'.

Wakiwa hawana habari, akili zao wakiwa wamezielekeza katika kuwazuia Olivier Giroud, Antoine Griezmann, Paul Pogba na Kylian Mbappe, vijana wa Roberto Martinez, walijikuta wakilizwa na mtu wasiyemtarajia kabisa. Sio wao tu, ulimwengu mzima haukumtarajia mwanaume yule mpole asiyekuwa na shida na mtu, kuichafua mikono yake kwa damu ya Wabelgiji wapatao milioni 11.

Haraka sana baada ya kumalizika kwa mchezo ule, nikiwa nimeridhika kuwa Ufaransa wametinga fainali, kama kawaida, nikawasha tarakilishi yangu na kuanza kazi ya kutafuta habari za muuaji yule. Katika kuperuzi hapa na pale, nikagundua kumbe yule muuaji aliyeitoa roho ya Ubelgiji, ni ndugu yetu kabisa.

Ni hivi, Novemba 14, mwaka 1993, katika hospitali moja mjini Yaounde, nchini Cameroon, mwanamama Annie Ngo Um, alijifungia mtoto wa kiume, na kwa mapenzi yake mwenyewe akaamua kumpa jina la Samuel Yves Umtiti. Msiniulize kuhusu baba yake maana hata Umtiti mwenyewe na umri wake wa miaka 24, haijui sura ya mwanaume huyo.

Mwaka 1995, Umtiti akiwa na umri wa miaka miwili tu, aliungana na kundi la wahamiaji haramu, walioingia Ufaransa. Haifahamiki kama Umtiti alisafiri na mama yake au la, kwa sababu, kumbukumbu zinaonesha kuwa, kutokana na ugumu wa maisha, Bi. Annie alimkabidhi Umtiti kwa jamaa yake amsaidie kumlea.

Katika kufika Ufaransa, aliweka makazi yake katika kitongoji cha Villeurbanne, Kaskazini Mashariki mwa mji wa Lyon. Baada ya kukaa miezi kadha Villeurbanne ambapo alilelewa katika jamii ya wahamiaji kutoka Cameroon, hatimaye walihamia Menival, kijiji kilichogundua kipaji cha Umtiti, ambaye ana ndugu yake aitwaye Yannick Umtiti, ila huyu sijui kama anacheza soka.

Historia ya beki huyu wa Barcelona inaonesha kuwa, alikuwa na mazoea ya kupita karibu na uwanja wa klabu ya Menival FC, bila kutarajia kale kaushetani ka kupenda soka ukauvaa moyo wake. Kila siku akawa anasimama pale uwanjani kwa dakika kadhaa, akiwa njiani kurudi kunako kambi ya wakimbizi, kushangaa mazoezi.

Alipotimiza miaka mitano, alianza kuonyesha ustadi wa kusakata gozi akiwa na miaka mitano hivi ambapo kwa makubaliano kati ya shule yake na mamake, kupitia kwa ndugu wa Mamake aliyekuwa anamlea (inasadikiwa ndiye aliyeondoka naye kwenda Ufaransa), Umtiti aliruhusiwa kuifuata ndoto yake.

 

 

Kwa mujibu wa Rais wa zamani wa klabu ya Menival  FC, Said Intidam, licha ya umri wake mdogo, Umtiti mgumu kama mnavyomuona, mkimya kama mnavyomuona, angeweza kucheza katika mechi ya wachezaji 11 kila upande bila matatizo. Ana roho ngumu balaa, sio ajabu mtu huyu huwa hacheki.

Mwaka 2001, akiwa na umri wa miaka tisa tu, alianza kwenda Lyon kujifunza soka na kuibuka kuwa miongoni mwa wachezaji nyota katika kikosi cha wachezaji chipukizi. Najua hujui ila nakufahamisha kuwa, Umtiti, alianza soka lake kama Straika, baadaye akawa anacheza safu ya kati kabla ya kuja kuwa beki kisiki.

Baada ya kukaa katika akademi ya Lyon akijifunza soka kwa zaidi ya miaka 11, Januari 2012, Umtiti alipandishwa hadi kikosi cha wakubwa cha klabu hiyo ambapo msimu wa 2015/16 alitawazwa mchezaji bora wa msimu na mashabiki wa klabu hiyo, akimgaragaza Alexandre Lacazette, anayekipiga pale  Arsenal, kwa sasa.

 

KUTAKIWA CAMEROON

Kutokana na kuzaliwa katika nchi ya Cameroon, Umtiti aliuwa na fursa ya kuichezea timu ya taifa ya nchi yake ya asili ambapo taarifa zinaeleza kuwa, Shirikisho la soka la Cameroon, wakimtumia Roger Milla ilifanya juhudi za kumpata beki huyo mwenye urefu wa futi sita (1.83m), ili aitumikie Indomitable Lions, lakini Umtiti aliweka ngumu.

 

KUJIUNGA NA BARCELONA

Baada ya kuonesha uwezo mkubwa katika kikosi cha Lyon, Barcelona walibisha hodi nchini Ufaransa, wakitaka saini yake. Juni 30, mwaka 2016, Umtiti akamwaga wino na kukubali kuhamia Camp Nou, kwa dau la Pauni milioni 25 (Sh 75 bilioni), akatua Camp Nou kuziba pengo  la Carles Puyol, aliyestaafu.

Mechi yake ya kucheza akiwa na uzi wa La blaugrana, ilikuwa ni Agosti 17, Kombe la Super Cup, wakashinda 3-0 dhidi ya Sevilla. Machi 4, mwaka 2017, akadunga bao lake la kwanza, katika mchezo wa ligi, dhidi ya Celta Vigo. Kadri siku zilivyosonga ndivyo alivyoendelea kuunda ushirikiano wa karibu na Gerard Pique na Jordi Alba.

 

KUICHEZEA LES BLUES

Umtiti aliitwa kuichezea timu ya taifa ya Ufaransa katika michuano ya Kombe la Euro 2016, iliyofanyika katika ardhi yao, akiingia katika kikosi cha Didier Deschamps, kuchukua nafasi ya Jeremy Mathieu, aliyeumia. Huo ndio ukawa mwanzo wa hadithi tamu ya Umtiti ndani ya uzi wa Les Blues.

Mechi yake ya kwanza ni mchezo wa robo fainali, dhidi ya Iceland, baada ya Adil Rami kupigwa 'Stop' kucheza mechi moja. Kiwango kizuri alichokionesha katika robo fainali, kilimpa nafasi ya kudumu kikosini. Kwa sasa ndiye mkoba wa Ufaransa, humwambii kitu. Ama kweli kufa kufaana!

 

 

Kitendo cha kucheza mechi yake ya kwanza katika michuano mikubwa na muhimu (wengine huanzia benchi au kwenye mechi za kirafiki) kilimaanisha kuwa, Umtiti anakuwa mchezaji wa pili katika historia ya soka la Ufaransa baada ya Gabriel De Michele, aliyechezeshwa kwenye Kombe la Dunia 1966.

Mpaka saza ameshaifungia Les Blues matatu ambapo bao lake la kwanza alifunga Juni 13, mwaka 2017, walipokutana na England mjini Paris na Ufaransa ikashinda 3-2. Kabla ya kuchezea timu ya wakubwa, Umtiti alikuwa katika kikosi cha timu ya vijana (U17 na U20) akiingia dimbani mara 47 na kufunga mabao matatu.

Huyo, ndio Mwafrika mwenzetu, mkimbizi Samuel Yves Umtiti, aliyewabeba Ufaransa na kuwapelaka fainali ya michuano ya Kombe la Dunia 2018, ambako watakutana na aidha wajukuu wa Malkia au vijana wa Madam Rais Kolinda Grabar- Kitalovic. Tukutane Luzhniki tukashangae mambo ya Samuel Umtiti.