Sijatenda haki najiuzulu – Hierro

Monday July 9 2018

 

Madrid, Hispania. Shirikisho la soka Hispania, limemshukuru aliyekua Kocha wa muda wa timu ya Taifa, Fernando Hierro aliyejizulu wadhifa huo juzi, akisema anawajibika kwa  kushindwa kuipa mafanikio katika fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia.

Hierro alipewa jukumu hilo siku mbili kabla ya kuanza harakati za kusaka taji la fainali za Kombe la Dunia 2018, akichukua nafasi ya Julen Lopetegui, aliyetimuliwa na Shirikisho hilo akiwa Russia, baada ya kukubali kuteuliwa kuwa Kocha wa Real Madrid.

Hata hivyo kuondoka Lopetegui kumeonekana kuwa pigo kuliko namna Shirikisho hilo lilivyodhani kwani Hierro, hakuweza kuivusha Hispania hata 16 bora.

Hilo lilikua pigo kwa mabingwa hao wa Dunia mwaka 2010 ambao hawakuonyesha soka la kuvutia katika fainali za mwaka huu kiasi cha kubezwa.

Hierro, mwenye miaka 50, amekataa pia kurudi katika nafasi yake ya awali ya Mkurugenzi wa Ufundi akisema anafikiria jambo jingine la kufanya.

Shirikisho la soka Hispania limelaumiwa sana kwa kumuondoa Lopetegui ambaye tangu ateuliwe kushika wadhifa huo mwaka 2016 baada ya kustaafu kwa Vicente del Bosque,  alikuwa hajashindwa hata mechi moja.