UCHAMBUZI: Migodi idhibitiwe maeneo ya hifadhi

Tanzania ni imejaliwa kuwa na utajiri wa madini ya aina mbalimbali katika maeneo mengi nchini.

Hata hivyo, bado uchimbaji wa madini katika maeneo hayo haujawanufaisha wachimbaji hasa wale wadogo kutokana na ukosefu wa teknolojia na mitaji.

Kutokana na wachimbaji wengi kutopata manufaa ya haraka, wengi wamekuwa wakiishi kwa kuhamahama kusaka maeneo ambako madini yanapatikana kwa urahisi.

Wachimbaji wadogo wameshindwa kuwekeza katika maeneo mengi na hivyo kila wanaposikia kuwa kuna eneo lenye madini hukimbilia huko kuchimba hata bila vibali.

Kwa sasa maeneo mengi rasmi yaliyogunduliwa kuwa na madini, wamepewa wawekezaji ambao wana mitaji ya kutosha na vifaa vya kisasa.

Hivyo, wachimbaji wadogo wamekuwa wakivamia maeneo mengine ambapo kuna dalili na fununu za upatikanaji wa madini na kuanza kazi.

Maeneo ambayo yamekuwa yakivamiwa na wachimbaji wadogo ni pamoja na hifadhi za Taifa na Hifadhi za Wanyamapori za Jamii (WMA).

Wachimbaji wanavamia maeneo licha ya kuwa yametunzwa kwa muda mrefu na yanatumika kwa shughuli za uhifadhi na utalii.

Katika hifadhi za Taifa za Manyara, Serengeti na maeneo ya hifadhi ya Makao wilayani Meatu zimekwishavamiwa.

Licha ya jitihada ambazo zinafanywa na wahifadhi, uroho wa utajiri wa haraka wa baadhi ya wachimbaji wamekuwa wakifanya uchimbaji wa madini kwa siri na tena nyakati za usiku.

Uchimbaji huu unachochewa na maofisa madini ambao tayari waliwahi kutoa vibali vya uchimbaji madini katika maeneo ya hifadhi.

Maofisa hao, kwa njia moja ama nyingine wamekuwa wakinufaika na uchimbaji huu holela ambao una athari kubwa kwa mazingira, uhifadhi na sekta ya utalii.

Hivi karibuni Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko na watendaji wa wizara hiyo walitembelea eneo la Makao WMA ambako zimebainika njama za kuvamiwa na kuchimbwa madini.

Pamoja na Biteko kupinga marufuku uchimbaji huo holela, pia aliagiza kuimarishwa ulinzi katika maeneo hayo ili kudhibiti uchimbaji wa madini katika maeneo yaliyohifadhiwa.

Hii ni hatua nzuri ya kusimama kidete na kuhakikisha maeneo ya hifadhi hayavamiwi. Ikiwa hali hii itaruhusiwa, athari zake ni kubwa kwa Taifa ambalo limekuwa likitegemea mapato ya utalii ambayo huchangia zaidi ya asilimia 18 ya Pato la Taifa.

Utalii pia umekuwa ukichangia zaidi ya asilimia 25 ya fedha za kigeni zinazoingizwa nchini, hivyo ni wazi jitihada zinahitajika kuwadhibiti watu wachache wanaotaka utajiri wa harakaharaka. Tatizo la uchimbaji madini pia lipo katika Hifadhi ya Manyara eneo la Magala ambapo yanapatikana madini aina ya alexandlite. Lakini licha ya kuelezwa athari za uchimbaji huo katika eneo la ikolojia ya Manyara - Tarangire bado kuna shinikizo la kuruhusiwa kwa migodi.

Hivyo itoshe kutoa wito kwa Serikali na wadau kushirikiana kuhakikisha maeneo ya hifadhi nchini yanaendelea kulindwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

Lakini pia ni muhimu sasa Wizara ya Madini ikafanya mapitio ya ramani ya jiolojia na kubainisha maeneo yenye madini ili wachimbaji wadogo wapelekwe kuchimba.

Katika maeneo hayo pia utaratibu wa kutolewa au kupatiwa mitaji na teknolojia za kisasa kwa bei nafuu, ungewekwa ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kutulia katika maeneo yao kuchimba madini na kulipa kodi.

Ni vizuri Serikali ikaendelea kuwadhibiti baadhi wa wachimbaji wenye nia ovu za kuvamia maeneo ya hifadhi za Taifa, mapori ya akiba na ya Hifadhi za Wanyamapori za Jamii (WMA) ili kuchimba madini.

Ni vizuri ikaeleweka kuwa kila kitu kati ya madini na utalii kina nafasi yake na umuhimu wake katika kuendelea na kukuza uchumi wa nchi. Hivyo jamii inatakiwa ijue kuwa hakuna sababu ya kuegemea upande mmoja na kuharibu upande mwingine.

Vilevile ni muhimu tuwe na vipambele kwa kuzingatia thamani hasa ya jambo tunalokusudia kufanya.

Kwa kuwa yapo maeneo ambayo yameainishwa kwa ajili ya uchimbaji madini na mengine yamebaki kwa ajili ya uhifadhi, kila moja lifanye kazi yake iliyokusudiwa bila kuingiliana.

Inapendeza pia hata taasisi za umma zinazohusika na maeneo hayo ziwe na mifumo inayoonana na inayofanya kazi pamoja ili kuepuka kutolewa kwa leseni zinazoingilia mamlaka za taasisi nyingine.

Mussa Juma ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Arusha; anapatikana kwa simu namba 0754-296503