UCHAMBUZI: Migodi ya madini Geita inachangia uharibifu wa mazingira

Mkoa wa Geita umebarikiwa kuwa na utajiri wa madini pamoja na machimbo mengi ya dhahabu nchini.

Kazi ya kuchimba madini ndiyo kiini cha mapato na shughuli nyingi za kiuchumi mkoani humo kuanzia kwa mtu mmoja, vikundi na wawekezaji wadogo na wakubwa.

Geita ni kati ya wilaya tano za mkoa huo na ndiyo kinara wa utajiri wa madini huku sehemu kubwa ikichimbwa na wachimbaji wadogo.

Pamoja na faida nyingi zinazotokana na sekta ya madini, pia zipo hatari na changamoto kadhaa zinazoambatana na utajiri huo.

Uharibifu wa mazingira ni kati ya changamoto kadhaa zinazoambatana na faida ya uwapo wa madini ya dhahabu Geita.

Ukataji wa miti kupisha uchimbaji na mashimo yanayotokana na kazi ya kuchimba madini ni miongoni mwa hasara ya kimazingira.

Madhara haya yameendelea na sasa uharibifu unaonekana katika maeneo ya misitu ambayo miti mingi imekatwa lakini hakuna jitihada za kupanda mipya.

Kwa mujibu wa ofisi ya Maliasili na Mazingira, asilimia 50 ya maeneo yenye shughuli za uchimbaji madini yameharibiwa kwa kukata miti kupisha migodi.

Msitu wa Ruande wenye ukubwa wa hekta 15,550 ni mojawapo wa misitu minne inayopatikana wilayani humo iliyoharibiwa kwa karibu asilimia 70.

Inakadiriwa kuwa hekta 10,885 zimeharibiwa kutokana na shughuli za kibinadamu.

Katika msitu wa Usindakwe wenye ukubwa wa hekta 450, zilizoharibiwa ni hekta 270, sawa na asilimia 60 huku hekta 19,080, sawa na asilimi 40 ya msitu wa Geita wenye ukubwa wa hekta 47, 700 zikiwa imeharibiwa.

Uharibifu huo pia upo katika msitu wa Rwamgasa wenye ukubwa wa hekta 15,500 huku zilizoharibiwa zikiwa ni hekta 4,650 (sawa na asilimia 30).

Kutokana na hali hiyo kuna hatari ya Mkoa wa Geita kuendelea kushuhudia uharibifu wa mazingira.

Wachimbaji wadogo wakiendelea kutegemea miti kwa ajili ya kutengeneza matimba ni dhahiri uharibifu utaongezeka kutoka asilimia 50 za sasa.

Christopher Kadeo, mwenyekiti wa wachimbaji wadogo mkoani Geita, anasema matumizi ya miti kwa lengo la kukwepa gharama za matumizi ya chuma kuwa ni miongoni mwa sababu za uharibifu wa misitu unaofanywa na wachimbaji wadogo.

Ukweli ni kwamba wachimbaji hawa hawawezi kujisimamia wenyewe, hivyo ni wajibu wa mamlaka na taasisi zinahusika na ulinzi na utunzaji wa mazingita kutimiza wajibu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Tuache kuingiza siasa kwenye masuala ya uhifadhi wa mazingira kwa kila mwenye wajibu kuzuia uvamizi na uharibifu wa maeneo ya hifadhi na misitu.

Ni vyema viongozi wa kisiasa wakaacha kutumia mamlaka na madaraka yao kuhalalisha uvamizi na uharibu wa misitu kwa sababu iwayo yote.

Tunapoelekea kwenye chaguzi za serikali za mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa 2020, kamwe tusitumie utetezi wa wavamizi na waharibifu wa misitu kama kete ya kisiasa kwa sababu kufanya hivyo ni hasara siyo tu ya kizazi chetu cha sasa, bali vizazi vijavyo pia vitaathirika.

Miongoni mwa madhara hayo ni kupotea kwa uoto wa asili, ukame, kukauka kwa vyanzo vya maji, kukosa mapato yatokanayo na uhifadhi na mwishowe umaskini.

Wakati umefika sasa kwa wanasiasa, wananchi, taasisi za mazingira, watendaji wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) pamoja na mamlaka zingine zenye dhamana ya kulinda na kuhifadhi misitu yetu kufanya kazi kwa karibu na kushirikiana kukabiliana na waharibifu wa misitu.

Wadau wa misitu wanapaswa kuwashauri viongozi na wanasiasa wetu kuhusu hatari na hasara ya mapendekezo, maelekeo na amri zao zinazokiuka sheria. Kiuhalisia, ni jukumu na wajibu wa kila Mtanzania mwenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kuhifadhi mazingira na misitu yetu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Rehema Matowo ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Geita anayepatikana kwa simu namba 0629-850 810