Mikakati ya utalii wa kiroho iungwe mkono

Tuesday July 10 2018

 

By ANTONY MAYUNGA

Tanzania ni nchi ya 91 kati ya nchi 136 duniani zenye vivutio vingi vya utalii. Hata hivyo, hali siyo nzuri katika kuboresha vivutio hivyo.

Kwa mfano, mbuga za wanyama sasa zimekuwa maeneo ya wafugaji wanaoingiza mifugo hasa ng’ombe ili kuchungia humo.

Kama hiyo haitoshi usalama, hali duni ya mawasiliano, miundombinu isiyoridhisha na tozo zisizokuwa rafiki kwa watalii vyote vinachangia kuzorotesha sekta hii muhimu.

Hata upande wa utalii wa utamaduni ambao sasa unashika kasi duniani hatufanyi vizuri licha ya kuwa na makabila zaidi ya 120 yenye kila aina ya utajiri wa mila, desturi na vitu vinavyoweza kuvutia watalii kuanzia wale wa ndani hadi wa nje.

Kutokana na changamoto hizo zinazoikabili sekta ya utalii hapa nchini ambayo kwa kiasi kikubwa inategemea zaidi utalii wa wanyama, kuna kila sababu kuwa na mikakati ya kukuza utalii wa aina nyingine.

Kwa mfano, baadhi ya mataifa yamepiga hatua zaidi katika utalii wa utamaduni na vivutio vya asili, lakini sisi licha ya utajiri mkubwa katika eneo hilo hatujafanya vizuri kama zilivyo nchi nyingine, kwa kuwa nguvu imeelekezwa kwenye utalii wa wanyama.

Tunatakiwa kuimarisha mikakati tofauti ikizingatiwa kuwa wanyama wanakabiliwa na changamoto kubwa hasa ya ujangili ambao unatishia baadhi ya viumbe hao kuelekea kwisha katika baadhi ya hifadhi na mapori ya akiba. Zipo nchi zinazofanya vizuri kwenye utalii wa mapumziko, biashara, mikutano, dini, utamaduni, historia na ule wa mazingira.

Serikali zao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zinatoa fursa kwa taasisi zenye uwezo kuanzisha aina za utalii zikiamini kuwa kufanikiwa kwa taasisi hiyo ni mafanikio kwa Taifa.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Utalii Duniani (UN-WTO), linaitaja China kuwa nchi namba moja kwa soko la utalii duniani, kutokana na idadi kubwa ya wakazi wa nchi hiyo kufanya utalii wa ndani.

Katika kuhakikisha utalii wa aina mbalimbali unafanyika hivi karibuni Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Michael Msonganzila akizindua nyumba ya tafakuri katika parokia ndogo ya Serengeti alisema hiyo ni hatua muhimu kwa kuwa nyumba hiyo inalenga kuimarisha sekta ya utalii.

Alisema kanisa hilo linakusudia kuanzisha utalii wa kiroho kwa ajili ya watalii kutoka ndani na nje ya nchi, baada ya kuonekana kuna hitaji hilo kwa makundi mbalimbali lakini haitolewi.

Huu ni ubunifu mpya ambao unatakiwa kupewa uzito na sekta za uhifadhi na wadau wake, kuhakikisha mkakati huo unazaa matunda bora, kwa kuwa una lengo lilelile la kuongeza huduma kwa wageni na wadau wengine wa utalii.

Ukweli ulivyo ni kuwa haiwezekani watalii wote wanaokuja Tanzania hasa wale wa kuangalia ikolojia kama ya Serengeti wasiwe na hitaji la kiroho. Na kama wanalo, wapi watapata huduma hiyo?

Mkakati huo ukifanikiwa katika ikolojia ya Serengeti kama lilivyo wazo la Askofu Msonganzila, tutakuwa katika nafasi nzuri ya kuusambaza katika maeneo mengine yenye fursa za utalii hapa nchini.

Leo hii kuna mamilioni ya watu wanaokwenda katika miji mitakatifu ya Makka, Madina na Jerusalemu kwa ajili ya mahitaji ya kiroho.

Bila shaka nchi husika zinaingiza kiasi kikubwa cha fedha kupitia watu hawa wanaofanya hija. Fursa kama hii inapaswa kuchangamkiwa hata hapa kwetu.

Kupitia utalii wa kiroho tunaweza kufungua fursa nyingi za utalii wa hija, kwa kuwa kuna maeneo mbalimbali hapa nchini yenye historia kubwa ya masuala ya dini, lakini mazingira hayajaboreshwa.

Ubunifu huu ni chachu ya maendeleo ikizingatiwa kuwa sekta ya utalii inakua kwa kasi huku ikichangia kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi.

Aidha, utalii ni chanzo cha fursa ya ajira kwa vijana wengi wanaoteseka, kutokana na hali ngumu ya maisha kwa kukosa fursa za ajira.

Utalii wa kiroho unawasaidia watu kufahamu vyema historia ya uumbaji na mchango wa maeneo hayo kiuchumi.

Unawajibisha kiutu na kimaadili ili watu waweze kuheshimiana, kuthaminiana na kuwa kikolezo cha maendeleo endelevu na utunzaji mazingira.

Utalii huo unajenga na kuimarisha mshikamano wa upendo na unasaidia kupunguza matendo yaliyo kinyume na maadili kwa jamii.

Pia, unadumisha utu katika ulimwengu wa utawandazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Hata mataifa yaliyofanikiwa kwenye utalii chanzo ni wazo, kisha mipango na mwisho utekelezaji wa pamoja kwa kuwa faida yake si ya aliyeanzisha wazo bali Taifa zima.

Antony Mayunga ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Mara 0787239480.