MTAZAMO: Mipango mikakati maendeleo ya soka letu haionekani

Monday May 13 2019Allan Goshashy

Allan Goshashy 

Inafahamika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ndiyo lina wajibu wa kuhakikisha kunakuwa na maendeleo ya soka nchini hasa katika suala la ufundi na elimu ya mchezo wa soka.

Maendeleo ya soka hasa katika suala la ufundi na elimu ya mchezo wa soka ni muhimu sana kwa soka la wanaume, wanawake na lile la ufukweni.

Ili, kupata maendeleo ya kweli ya mchezo wa soka, kuna mambo manne ya kuzingatia ambayo ni: kwanza ni elimu kwa makocha, maendeleo na suala la leseni kwa klabu, pili ni elimu kwa waamuzi na maendeleo yao, tatu ni mipango mikakati ya kuendeleza soka ndani ya TFF na nne ni maendeleo ya suala la matibabu kwa wanamichezo pamoja na utafiti.

Mambo haya manne hayafanyiki nchini kwa kiwango kinachotakiwa. Kama yangekuwa yakifanyika kwa kiwango kinachotakiwa yangekuwa yakionekana kwa kiwango cha juu kabisa.

Hebu angalia kiwango cha elimu kinachotolewa kwa makocha wetu chini ya usimamizi wa TFF. Jiulize, je, makocha wetu wazawa wana kiwango cha elimu ya mchezo wa soka kama inavyotakiwa? Jiulize tu, waamuzi wetu wana elimu ya kutosha ya mchezo wa soka? Je, waamuzi wetu wanapata nafasi za kuchezesha mashindano ya kimataifa?, Je, kuna mpango mkakati wa kuendeleza soka ambao upo chini ya TFF? Je, mpango huo unaeleweka kwa wananchi na wadau wa soka nchini?

Hakika kuna maswali mengi sana kuhusu maendeleo ya soka nchini hasa katika suala la ufundi na elimu ya mchezo wa soka.

Mtazamo wangu,TFF inatakiwa kukaa chini na wadau mbalimbali wa soka nchini, makampuni, CAF pamoja na FIFA ili kuangalia namna ya kuleta maendeleo ya soka nchini hasa katika suala la ufundi na elimu.