UCHAMBUZI: Miradi hutekelezwa kulingana na rasilimali zilizopo

Kuwa na uwezo wa kufanya uamuzi wa matumizi pale rasilimali zinapokuwa chache kuliko mahitaji ni busara inayotumiwa na wengi.

Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa, wakati wote wa kuishi kwa mwanadamu, mahitaji huwa mengi kuliko rasilimali alizonazo kutekeleza haja za moyo wake.

Ingekuwa rasilimali zinatosheleza kila wakati pengine pasingekuwa na tija ya kaya, jamii au Taifa kwa ujumla kuwa na malengo ya muda mfupi, kati na mrefu.

Tunafikia hatua ya kuweka malengo ili kujipa muda wa kukusanya rasilimali za kutekeleza malengo husika kwa njia halali zinazokubali kwenye jamii.

Baadhi ya malengo kwa sababu ya ukosefu wa rasilimali huahirishwa ili kujipa muda wa kukusanya na kufanya tathimini kabla ya kuamua kuendelea nayo au kuachna nayo.

Ili kufanya uamuzi sahihi takwimu pekee hutumika kuhalalisha utekelezaji au uhairishaji wa malengo yaliyopo licha ya ushawishi wake kwa wakati uliopo.

Kwa mfano, familia inaweza kupanga kujenga nyumba, kupeleka mtoto kusoma nje ya nchi au kununua gari jipya. Endapo kaya hiyo haitakusanya rasilimali za kutosha kutekeleza hayo yote, inaweza kuahirisha kujenga nyumba na kununua gari ili kumsomesha mtoto.

Pengine sababu kubwa ya kutekeleza lengo la pili ni kutimiza msemo wa urithi bora kwa mtoto ni elimu wakati hayo mengine yakisubiri mipango ikae sawa baada ya muda.

Malengo yaliyosalia kama kaya itaona bado yana umuhimu inaweza kusogeza mbele utekelezaji wake au kuondoa na kuweka mengine kutokana na mahitaji na uwezo wa kukusanya rasilimali uliopo.

Haya hutokea lakini wakati mwingine linaweza likajitokeza jambo muhimu zaidi hata mawazo yote matatu yakaachwa. Chukulia baba au mama ameugua ghafla na anahitaji matibabu yanayogharimu sawa na ada ya mtoto…afya ya mzazi huyo inaweza kupewa kipaumbele

Baadhi ya watumishi wa umma walikuwa na matumaini makubwa ya Serikali kutangaza ongezeko la mshahara mwaka wa fedha 2018/19. Hilo halikufanyika kwa takwimu ambazo Rais John Magufuli alizitumia kutetea uamuzi wa Serikali yake.

Pamoja na mambo mengine alieleza kwa sasa Serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha miundombinu ya uchumi ili mkulima, mfugaji, mvuvi na mfanyakazi aweze kunufaika kwa mapana zaidi.

Ipo miradi inayoendelea ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa, mradi wa umeme Mto Rufiji, uimarishaji wa usafi wa anga, ujenzi wa barabara, upanuzi wa bandari, ujenzi wa madaraja na vivuko mbalimbali.

Miradi hii inahitaji fedha nyingi kabla haijakamilika na kuanza kutua hudumu iliyokusudiwa. Kwa mfano, miradi miwili ya ujenzi wa reli na wa kufufua umeme Mto Rufuji (Stiegler’s Gorge) inatarajiwa kutumia ziadi ya Sh10 trilioni hadi kukamilika kwake.

Takwimu zinaonyesha baada ya kuondoa watumishi wa umma wasio na sifa, Serikali inatumia wastani wa Sh564.5 bilioni kulipa mishahara kwa watumishi wa kila mwezi.

Wakati huo huo, takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinaonyesha makusanyo ya kila mwezi ni wastani wa Sh1.2 trilioni. Hii ina maana kuwa Serikali inatumia zaidi ya asilimia 47 ya makusanyo kulipa mishahara kwa watumishi wa umma kila mwezi.

Wastani wa asilimia 53 inayobaki inaelekezwa kugharimia utaoaji wa elimu bila malipo katika shule zote za msingi na sekondari, mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, kuimarisha huduma za afya, maji, kilimo, mifugo na uvuvi. Vilevile, kulipa deni la Taifa, kuimarisha na kujenga miundombinu ya barabara na anga.

Nchi inapotekeleza miradi mikubwa ya aina hii ndipo dhana ya kupanga ni kuchagua inapohitaji kutumika kwa maslahi mapana ya wananchi wote. Ni wananchi hao watakaonufaika pindi ikikamilika baada ya kero walizokuwa wanakabiliana nazo kutokuwapo tena.

Kiuchumi, riba inayotozwa katika huduma za fedha haiwezi kuwa chini ya kiwango cha mfumuko wa bei. Tija ya ongezeko la mshahara bila kudhibiti mfumuko wa bei ni sawa na kujaza maji kwenye pakacha.

Mfumuko wa bei unapokuwa madhubiti unamuwezesha mlaji kutumia kiasi kidogo cha fedha kupata huduma nyingi zaidi anazozihitaji. Unapokuwa na rasilimali chache na mahitaji mengi ni lazima takwimu zielekeze ni kipi cha kuanza na kipi kifuate baadae kama bado kuna ulazima wa kufanya hivyo.

Mwandshi ni mtakwimu na ofisa mipango. Ni mtumishi wa Serikali.