UCHAMBUZI: Mitandao ya kijamii ni fursa, usiitumie kwa kupiga porojo

Simu yako ya mkononi ni zaidi ya kifaa unachoweza kukitumia kuwasiliana na ndugu, jamaa na marafiki. Kinakuwa na maana zaidi pale inapokuwa simu janja (smartphone) kwani kwa kujiongeza unaweza kufanya mengi.

Matumizi ya simu hizi ambazo wataalamu hupenda kuziita kompyuta ndogo yameleta mabadiliko katika utangazaji duniani.

Kwa mfano kuwa na biashara au kutoa huduma ni suala moja na kuwafikia wanaohitaji kununua au kuifahamu ni suala lingine.

Hivyo wakati unaboresha bidhaa au huduma zako fikiria pia kuwafikia wateja wako kwa kutumia mbinu mbalimbali kadri uwezavyo.

Hapo awali ilikuwa changamoto kuwafikia wateja wanaohitaji huduma yako au bidhaa zako, kwa sababu ulilazimika kununua muda wa matangazo kwenye redio, runinga au magazeti, lakini sasa uwezo huo upo kiganjani kwako.

Kupitia mitandao ya kijamii, hata kama utalazimika kulipa itakuwa ni kiasi kidogo, ukilinganisha na ilivyokuwa kwa njia hizo nilizozitaja hapo awali.

Kwa kutambua matangazo ni sehemu muhimu ya biashara, jipange namna ya kutumia mitandao kufanikisha hilo.

Huna haja ya kuwa na kompyuta au simu ya gharama kuweza kufanikisha haya. Unachohitaji ni simu janja ya gharama yoyote na mtandao tu.

Tofauti na wenye umri mkubwa ambao watalazimika kuajiri mtu kwa ajili ya kufanya kazi, wewe kama kijana suala hilo ni rahisi kwako.

Utaratibu ni rahisi mno, anza na marafiki ulionao katika kurasa zako za mitandao ya kijamii, hakikisha unawashawishi na wao wanaweka kwenye kurasa zao.

Unaweza kuwashawishi kwa kubadilishana nao bidhaa, wakiweka za kwako na wewe siku moja moja unaweka za kwao.

Kutangaza kwa kutumia mitandao ya kijamii kunahitaji uwe na marafiki wengi wanaotembelea kurasa zako, hivyo si vibaya ukachagua aina fulani ya habari ukawa unaweka ili kuvutia watu.

Hapa nchini watu wanapenda kusikia habari za watu hususani maarufu, unaweza kuposti habari za mastaa ulizozisikia au kuziona.

Unaweza pia kuzitoa kwenye mitandao ya marafiki zako na kuiweka kwako, watu watakuja kwa ajili hiyo, usisahau kutaja ulikotoa hizo habari za mastaa ikiwa ni heshima kwao.

Kuna watu wanataka habari lakini hawazipati kutokana na kuwa na shughuli nyingi, ukiwaletea kupitia mitandao hiyo wataipata kwa urahisi kupitia simu za mkononi.

Hivyo badili matumizi ya mitandao haswa Instagram, Facebook na Whatsapp ambayo inafuatwa na watu wengi badala ya kuitumia kupiga soga itumie kujiongezea kipato.

Ukiwa na marafiki wengi wanaotembelea kurasa zako, unaweza pia kufanya matangazo ya bidhaa za watu wengine kwa malipo nafuu.

Kadri unavyofanya matangazo ya bidhaa zako vizuri, ndivyo utakavyowavutia wengine kutangaza nawe na mpangilio wako utavutia watazamaji ambao kimsingi ndiyo wateja.

Utaongeza watu kwa sababu watakaovutiwa nawe watakutangaza na kuwaita wengine kuja kwenye kurasa zako kuangalia bidhaa bora unazotangaza na mpangilio bora wa utangazaji usiochosha.

Njia hii pia inaweza kukuandaa kupata kipato cha haraka haraka na cha baadaye.

Utajenga vipi kipato cha baadaye?

Jibu ni kama una ujuzi , ufahamu wa jambo fulani hata kwa kiasi kidogo, tumia muda mwingi kuwapa wanaotembelea kurasa zako elimu ya jambo unalolifahamu.

Unapotoa elimu hiyo usiwe na haraka ya kuona mafanikio, hakikisha wamekuzoea na wanahitaji huduma yako, utalipima hili kutokana na maswali utakayokuwa unaulizwa faraghani na kwenye kurasa zako.

Ili uhitaji uwe mkubwa tafuta jambo unalolifahamu vizuri, usiwe na mzaha katika taarifa unazotoa, hii itawaongezea hamu ya kutaka kusikia utawaletea mada gani baada ya hiyo wanayoisoma au kuiangalia wakati huo.

Hapo badili mfumo na kuanza kuwatoza fedha kwa kuunda kundi la Whatsapp la watu wachache na kuwapa elimu kwa kulipia.

Hakikisha wale wengine huwaachi na ikiwezekana wote wahamie kundini kwa kuendelea kuwashawishi kupitia mitandao ya Whatsapp, Facebook na Instagram.

Jiulize kila siku, kiasi cha fedha ulichotumia kununua data kinaakisi ulichopata katika mtandao. Iwe maarifa mapya au fedha.

Usikubali kuwa miongoni mwa wengi wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuwashambulia watu au kutazama vitu visivyo na tija kwa afya ya ubongo.