MAONI: Mkakati uwekwe kunusuru uchumi na corona

Tuesday March 31 2020

Dunia ni kama imesimama wakati huu ambao ugonjwa wa virusi vya corona unasambaa kwa kasi kila kona.

Uchumi wa dunia uko katika hatari ya kuporomoka kutokana na serikali za nchi mbalimbali kupiga marufuku mikusanyiko, kuzuia wageni kuingia, na hata kuzuia wananchi wake kutoka majumbani kujaribu kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo ulioua zaidi ya watu 34,600 na kuambukiza zaidi ya watu 700,000.

Uamuzi kama huo hauwezi kuziacha salama biashara. Biashara zimeathirika, baadhi ya kampuni zikipunguza shughuli zake na nyingine kufungwa, mashirika ya ndege yamesimamisha safari, michezo imesimama na athari zinaendelea kusambaa katika nyanja nyingi siku hadi siku.

Ajira zinapungua na inakadiriwa kuwa watu wasio na kazi wataongezeka kutoka milioni 5.3 hadi kufikia watu milioni 24.7 (kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani, ILO).

Tanzania, na nchi nyingine za ukanda huu, haziwezi kukwepa anguko hilo iwapo ugonjwa huo unaoshambulia mapafu, hautadhibitiwa mapema. Tayari hoteli na baadhi ya biashara ama zimepunguza shughuli au zimefungwa kutokana na kukosa wateja, ambao ama wanakosa ndege za kuwaleta, au wanazuiwa kutoka nchi zao au hawawezi kumudu gharama za kukaa kwa siku 14 bila ya kutimiza malengo yanayowaleta kutokana na kuwekwa karantini hotelini kwa gharama zao.

Kwa nchi ambayo haina huduma bora za afya kama vitendea kazi vya kisasa na vya kutosheleza mahitaji hospitalini na miundombinu, sala kuu ugonjwa huo usiingie kwa kasi ile ulioingia nao katika nchi tajiri duniani kama Italia, Ufaransa, Hispania, Marekani na Korea Kusini ambazo zina nyenzo za kupambana nao lakini zimeathirika sana.

Advertisement

Sala hiyo inaendana na wananchi kufuata maelekezo yote yaliyotolewa na wataalamu kuhusu jinsi ya kujikinga na pia watendaji wa serikali kutekeleza kwa uadilifu kazi yao ya kudhibiti wageni ili wasiingize maambukizi ndani ya nchi.

Wakati jitihada hizo zikiendelea, ni lazima kujua kuwa maisha yataendelea baada ya dunia kudhibiti mlipuko wa virusi vya corona. Yataendelea kwa biashara kurejea katika hali ya kawaida na hivyo uchumi wetu kurudia uimara wake.

Ndio maana nchi tofauti sasa zinafanyia kazi sera zake za kifedha kuona zitafanyaje ili kuokoa sekta ya umma na binafsi katika hatari ya kuanguka, baadhi zimetenga fedha kwa ajili ya kusaidia kampuni, nyingine zina mpango wa kununua sehemu kubwa ya hisa za kampuni kubwa na nyingine zinabeba mzigo wa kufidia wanaopunguzwa kazini kwa muda.

Hapa nchini, utalii, ambao umekuwa kinara katika kuingiza fedha za kigeni, ndio ulioathirika sana kwa kuwa hakuna watu wanaosafiri kutoka nchi zao kuja nchini. Hoteli na shughuli zinazohusiana na utalii zinafungwa, na maelfu ya ajira pia kutoweka.

Wakati huohuo, Serikali pia inahitaji makusanyo ili iweze kuendesha shughuli zake za kuwahudumia wananchi na kuwajengea miundombinu ya kurahisisha kazi zao. Katika hali hiyo, mlipuko wa virusi vya corona unaiweka nchi katika hali ambayo ni ngumu kufanya uamuzi unaosaidia sehemu tofauti.

Kitu kizuri ni kwamba wote walioona athari za baadaye za mlipuko huo wameanza kutoa kilio chao serikalini wakitaka watupiwe jicho la ziada ili wasije wakafunga shughuli zao, wakianzia na wamiliki wa hoteli.

Hao ni wachache. Kadri siku zinavyokwenda wataibuka wengi zaidi kutoa kilio hicho na mapendekezo tofauti ya nini cha kufanya.

Ni matumaini yetu kuwa Serikali itakusanya vilio na mapendekezo hayo na kuja na mkakati utakaonusuru uchumi na maisha ya wananchi wote.