Mkuu wa Mkoa Dar aheshimu sheria zilizopo

Tuesday February 13 2018

 

Tumeshtushwa na tamko la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda la kusitisha mabaraza yote ya ardhi ya kata katika mkoa pamoja na kesi zote hadi utaratibu wa kupitia upya taaluma za wanasheria waliopo kwenye mabaraza hayo utakapofanyika.

Mbali ya kusitisha mabaraza na kesi aliwaagiza makatibu tarafa wote kutembelea mabaraza hayo na wakurugenzi wa halmashauri wampatie wasifu wa wakuu wa idara na kazi wanazofanya.

Vilevile aliagiza madalali wa mahakama kufika ofisini kwake leo wakiwa na nyaraka za usajili ili wafahamike akisema wapo baadhi ambao wanapindisha sheria na utaratibu.

Tunafahamu kuwa lengo la mkuu huyo wa mkoa ni zuri lakini ieleweke yeye kama mkuu wa mkoa kisheria hana jukumu katika mfumo wa utoaji haki na kwamba mahakama zinatakiwa kuwa huru bila kuingiliwa na mamlaka nyingine ya nje.

Tunaposoma nyaraka mbalimbali kuhusu muundo wa mabaraza ya ardhi ya kata tunachelea kusema amekiuka sheria kwani nyaraka zinaonyesha wazi mabaraza haya yalianzishwa kwa Sheria ya Mabaraza ya Kata mwaka 1985 chini ya sheria namba 7 ili kusaidia kutatua migogoro ya kijamii inayotokea katika kata husika.

Sheria hiyo iliongezewa nguvu kwa Sheria ya Ardhi ya Kijiji ya Mwaka 1999 na baadaye Sheria ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi ya Mwaka 2002 ili pia yaweze kusikiliza mashauri ya ardhi.

Mamlaka ya Baraza la Kata kwa mujibu wa Sheria ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi ya mwaka 2002 ni kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi iliyotokea katika kata husika. Mabaraza ya Kata, ambayo husimamiwa na Wizara ya Nyumba na Ardhi husikiliza mashauri ya ardhi yenye thamani ya ardhi isiyozidi Sh3 milioni.

Mabaraza haya pamoja na kazi nyingine yanasuluhisha migogoro ya ardhi kwa kufuata mila na desturi za mahali, kanuni za haki asilia au taratibu ambazo wajumbe wamefundishwa katika mafunzo yao.

Sheria hiyo inasema upande ambao unakuwa haujaridhika una haki ya kukata rufaa ndani ya siku 45 baada ya uamuzi kutolewa kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya. Nyaraka zinabainisha wazi kwamba kwenye Baraza la Kata, wakili haruhusiwi kuwakilisha wateja.

Tunafahamu kwamba kuna matatizo katika usuluhishi au utatuzi wa migogoro hiyo ndiyo maana kuna malalamiko mengi na kesi nyingi mahakamani. Tunatambua zinahitajika juhudi za ziada za usimamizi, uaminifu na uharaka katika utatuzi wa migogoro hiyo.

Hata hivyo, ufumbuzi wake hauwezi kuwa ni kusimamisha shughuli za mabaraza ya kata ambayo yaliundwa kisheria. Kama kuna tatizo katika muundo wake ni vyema mkuu wa mkoa ambaye yumo katika serikali inayofanya juhudi kutatua kero mbalimbali, tena kwa haraka, akafanya ushawishi uandaliwe muswada wa marekebisho ya mabaraza hayo badala ya kutoa tamko lisilo la kisheria.

Hivi mkuu wa mkoa hana habari kwamba mahakamani kuna kesi nyingi na watu wengine wamekaa muda mrefu bila kesi zao kusikilizwa? Kama zipo, mbona shughuli za mahakama hazisimamishwi hadi wasifu wa mahakimu au majaji upitiwe?

Tunamshauri mkuu wa mkoa na wengineo watumie wanasheria waliomo kwenye ofisi zao kupata ushauri wa kisheria ili wasijikute wanaingilia wizara au mihimili mingine au kuzua migongano ya kisheria.