MAONI: Mkwamo bei ya pamba upatiwe suluhisho la kudumu

Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ilijinadi na kaulimbiu ya Tanzania ya viwanda.

Baada ya ushindi, Rais Magufuli aliendelea kusisitiza azma hiyo huku akiwataka Watanzania kumuunga mkono.

Ni ukweli ulio wazi kwamba ili azma ya Serikali ya viwanda ifanikiwe, kilimo kamwe hakiwezi kuwekwa kando, ni lazima juhudi zifanyike kuhakikisha malighafi za viwandani zinapatikana kwa wingi.

Malighafi hizo zinaweza kuagizwa nje lakini litakuwa jambo la busara kama malighafi hizo zikitoka ndani, kwa maana ya kwamba wakulima wa Tanzania wawezeshwe ili kilimo chao kiwe na tija na chenye mchango mkubwa katika viwanda vya ndani.

Tunalisema hili tukiamini kuwa wakulima wakiwezeshwa wataweza kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa viwanda ambao Serikali ya awamu ya tano imejinadi kuusimamia.

Katika kulifanikisha hilo ni vyema Serikali ikahakikisha matatizo ya hapa na pale yanayowakwaza wakulima hususan suala la bei ya mazao yanatafutiwa suluhisho la kudumu ili waone matunda ya kilimo chao na kilimo hicho kiwe na mchango katika uchumi wa viwanda.

Kwa mfano hatuoni ni kwanini wakulima wa pamba wanapata wakati mgumu kuuza zao lao kutokana na tatizo la bei wakati Serikali yenye nia ya kuanzisha viwanda itahitaji pamba kama malighafi viwandani.

Juzi Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa wilayani Igunga mkoani Tabora alitangaza kupatikana ufumbuzi wa bei ya pamba ya Sh1,200 kwa kilo baada ya awali wanunuzi kusita kununua pamba baada ya bei ya zao hilo kushuka kwenye soko la dunia.

Ufumbuzi huo ulipatikana baada ya Waziri Mkuu kufanya kikao na wanunuzi wa pamba, wakuu wa mikoa inayolima zao hilo, wawakilishi wa mabenki pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Baada ya kikao hicho, BoT walikubali kudhamini mikopo ya wanunuzi wa zao hilo katika mabenki na taasisi za fedha nchini na hivyo kuwaondolea hofu wanunuzi wa pamba ambao hatimaye walikubali kununua zao hilo kwa bei elekezi ya Sh1,200.

Hatua alizochukua Waziri Mkuu ni za kuungwa mkono lakini ni vyema ufumbuzi wa aina hii ukawa wa kudumu ili kuwapa wakulima matumaini ya kupata fedha zao kwa wakati.

Na hili lisiwe tu katika pamba, iwe hivyo hata kwa mazao mengine, suala la bei lisimamiwe vizuri na suluhisho lake liwe la kudumu, isitokee tena msimu ujao wa pamba au zao jingine kukawa na mkwamo wa bei.

Mkwamo wa bei si tu unawakwaza na kuwakatisha tamaa wakulima bali unakwamisha azma ya Serikali ya kuwa na Tanzania ya Viwanda, mafanikio katika viwanda yanahitaji kuungwa mkono na juhudi za kwenye kilimo.

Na katika hili kwa siku zijazo ni vyema Serikali ikashirikisha wadau ili badala ya kuuza pamba, Tanzania ianze kuzalisha mali zinazotokana na zao hilo, kuanzia nyuzi, nguo na bidhaa nyinginezo zinazotokana na mazao ya kilimo.

Tunaamini haya yakiwekewa mkazo yatawezekana na matunda yake yataonekana na ile azma ya uchumi wa viwanda itakuwa na maana zaidi kwa wananchi walio wengi.