Mloganzila itumie vizuri fedha ilizopewa

Tuesday June 12 2018

Juzi, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan aliamua kuiongezea fedha Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Mloganzila ya Dar es Salaam kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya upungufu wa dawa.

Aliamua kuongeza fedha hizo kutoka Sh600 milioni hadi Sh900 milioni na kuutaka uongozi uzitumie vizuri kusudi ziwaondolee kero wananchi wanaofika kutibiwa hospitalini hapo.

Hatua ya kuongeza fedha hizo imekuja baada ya siku za hivi karibuni kuwapo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wagonjwa wanaodai kukosekana kwa baadhi ya dawa katika hospitali hiyo.

Tunampongeza Makamu wa Rais kwa kuifanyia kazi kwa haraka changamoto hiyo na pia tunaungana naye kuutaka uongozi wa hospitali hiyo utumie vizuri fedha utakazozipata kulipia huduma hiyo Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo.

Tunasema hivyo kwa kuwa kumezuka tabia kwa baadhi ya hospitali, zahanati na vituo vya afya vya Serikali kushindwa kulipa fedha za dawa wanazouziwa na MSD, licha ya kuwa dawa hizo mbali ya kutengewa bajeti, zinawaingizia fedha ambazo wanaweza kuzitumia kulipa madeni na kuagiza dawa zaidi bila kuacha deni na malalamiko kwa wananchi.

Kwa mujibu wa kauli ya uongozi wa MSD kwamba haina upungufu wa dawa na kwamba huzisambaza katika hospitalini, vituo vya afya na zahanati kulingana na kiwango kinachoagizwa na wahusika, maana yake ni kuwa hatutarajii kusikia malalamiko ya kukosekana kwa dawa katika hospitali hiyo.

Hivyo, ifike mahali huu wimbo wa ukosefu wa dawa unaoimbwa na wananchi kila uchao katika hospitali zetu nchini umalizwe kwa kuanza kutathmini matumizi na idadi ya dawa zinazoagizwa ili kuona kama zinakidhi mahitaji.

Tumemsikia pia Makamu wa Rais akimwagiza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aiongezee hospitali hiyo Sh300 milioni ili kuiwezesha ijiendeshe na kupunguza changamoto mbalimbali inazokabiliana nazo, kama hiyo ya upungufu wa dawa.

Tuna imani kuwa agizo hilo litazingatiwa na fedha zitakazoongezwa pia zitafanya kazi iliyokusudiwa na hatutarajii kusikia ongezeko la malalamiko ya wananchi dhidi ya kero, hususan ya kukosa huduma na nyingine zilizo ndani ya uwezo wake.

Hakuna shaka kwamba ikiwa uongozi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Mloganzila utatekeleza kile kilichoagizwa na Makamu wa Rais, hakuna ambaye atawanyooshea kidole tena.

Msisitizo wetu mkubwa kwa uongozi wa Hospitali ya Mloganzila ni kulipa bili zake za MSD kwa wakati. Tayari Serikali imeiongezea fedha hivyo kama inadaiwa na MSD ilipe bili na iagize dawa zaidi hata zile ambazo haizipati kutoka serikalini.

Itafanikiwa katika hilo pale tu itakapofungua duka lake la dawa ambalo litaweka aina nyingine za dawa itakazonunua kupitia wakala mbalimbali na si Bohari Kuu ya Dawa.

Tunatoa rai pia kwa wananchi kuchangia huduma za matibabu kupitia bima za afya ili waweze kupata matibabu ya kibingwa ya ngazi za juu bila vikwazo.

Kwa sababu Mloganzila ni miongoni mwa hospitali saba zinazomilikiwa na Serikali zinazotoa matibabu ya kibingwa ngazi ya juu na uwapo wake umeleta unafuu katika kuongeza wigo wa huduma na mafunzo kwa wataalamu wa afya na huduma za matibabu kwa wananchi, tunaamini kwamba Watanzania watazifurahia huduma zake.