Msaada huu sawa, lakini utazamwe upya

Muktasari:

  • Pamoja na nia njema ya Serikali ambayo hatuna budi kuipongeza, tumesikitishwa na uamuzi uliotangazwa na mkuu wa wilaya hiyo, Moses Machali kuwa mwalimu huyo anajengewa nyumba ya miti ambayo itawezesha kuishi walimu wengine watakaoongezwa.

Miongoni mwa habari zilizotia faraja wiki ni ile ya kumjengea nyumba Bosco Chilumba, mwalimu pekee katika shule ya msingi Chikotwa wilayani Nanyumbu.

Mwalimu huyo anayefundisha jumla ya watoto 99 kuanzia darasa la awali hadi la tano amekuwa mfano pekee wa kujituma katika mazingira magumu hadi uongozi wa wilaya hiyo ukamwona baada ya kumulikwa na gazeti hili.

Kutokana na habari hiyo, uongozi wa Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara kwa kushirikiana na jeshi la akiba na wananchi wa kitongoji cha Chikotwa, wameanza ujenzi wa nyumba ya mwalimu huyo.

Pamoja na nia njema ya Serikali ambayo hatuna budi kuipongeza, tumesikitishwa na uamuzi uliotangazwa na mkuu wa wilaya hiyo, Moses Machali kuwa mwalimu huyo anajengewa nyumba ya miti ambayo itawezesha kuishi walimu wengine watakaoongezwa.

Tunajua kuwa zipo changamoto mbalimbali kiuchumi katika halmashauri, Serikali na kwa wananchi, lakini tunadhani bado kuna uwezekano wa mwalimu huyo kujengewa nyumba ya kisasa zaidi kwa kutumia matofali.

Tungependa msaada huu anaopewa mwalimu huyo na wengine wanaotarajiwa kuhamishiwa hapo kusaidiana naye wapate makazi ya kisasa yanayostahili kwa kazi iliyotukuka wanayoifanya.

Kazi ya mwalimu huyo sio ya kubeza, ni ngumu ambayo imewashinda wengine wengi waliopo katika mazingira ambayo hayana changamoto kama hizo.

Yaani mwalimu mmoja huyohuyo aandae somo kwa kila kipindi kwa madarasa yote, afundishe, atoe kazi za nyumbani, asahihishe kazi za wanafunzi, atunge mitihani na kuisahihisha pamoja na kupanga matokeo.

Si hayo tu, mwalimu huyo asimamie nidhamu, usafi wa mazingira, madarasa na wanafunzi wenyewe na baada ya kazi aende nyumbani kupumzika na kupata usingizi. Hakika mwalimu huyu anastahili kulala sehemu iliyotulia, zaidi ya nyumba ya miti inayoweza kusaidia afya ya akili yake kuimarika.

Ni imani yetu kuwa zaidi ya kumpatia mwalimu huyo makazi bora zaidi itakuwa ni kichocheo na kivutio cha walimu wengine kukubali kwenda katika shule hiyo kuongeza nguvu kuwaelimisha watoto hao.

Pamoja na kwamba mpango wa ujenzi huo umepangwa kuchukua wiki mbili, tunashauri uongozi wa wilaya hiyo ukune kichwa zaidi au uhamasishe wananchi wachangie kupata hata nyumba moja ya kuanzia ikiwa na ubora zaidi.

Tunaamini Mwalimu Bosco ambaye ameshukuru kwa hatua zilizochukuliwa siku akipata nyumba bora zaidi atashukuru maradufu na kuongeza juhudi zaidi.

Na ikitokea hali hiyo, mafanikio ya mwalimu huyo hayataishia kuwawezesha wanafunzi wake kuanzia darasa la pili hadi la tano kujua kusoma na kuandika, bali anaweza kutoa wengi kwenda sekondari na baadaye kupata wataalamu.

Kwa sasa kati ya wanafunzi hao, wawili tu ndio wanasoma kwa ‘kuungaunga’ maneno na hata matokeo ya mtihani wa darasa la nne mwaka jana wanafunzi wote walifaulu na kuingia darasa la tano.

Vilevile tunashauri juhudi za wilaya na halmashauri zisiishie kwenye nyumba ya mwalimu, bali pia ziongezwe katika ujenzi wa vyumba ili kila darasa lisome peke yake.

Kwa sasa Chilumba (33), anafundisha darasa mojamoja kwa zamu huku kipaumbele zaidi kikiwa ni la kwanza na pili ili wajue kusoma na darasa la nne kwa sababu ya mtihani wa kitaifa. Bila shaka watakapofika darasa la saba hali itakuwa mbaya zaidi, maana wanaohitaji kipaumbele wataongezeka, hivyo juhudi zaidi za kiserikali zinapaswa ziongezeke.