Msitu wa Nyumbanitu wenye simulizi za ajabu- 2

Kiongozi wa msitu huo, Julius Msigwa, akionyesha ishara ya kuwaruhusu wageni kuingia msituni.

Muktasari:

MSITU WAFYEKWA

Kwa wenyeji wa Mkoa wa Njombe, wanajua kuwa msitu huu umezungukwa na misitu wa miti iliyopandwa na Kampuni ya Miwati (Tanwat).

Julius anasema Chifu Mkongwa aliwasiliana na Tanwat kupanda misitu kwenye maeneo ya kuzunguka msitu huo wa asili ili wananchi wake wapate ajira.

“Lakini, kwa bahati mbaya wakati wa upandaji wa miti, kampuni hiyo iliamua kufyeka msitu wa Nyumbanitu ili siku ya pili, ije kupandwa miti ya Miwati kwa ajili ya matumizi ya kampuni,” anasema.

“Msitu mzima ulifyekwa na kulimwa. Cha ajabu siku ya pili walipokuja kwa ajili ya kupanda miti yao, walishangaa kuona msitu haujaguswa. Upo vilevile.”

Julius anaongeza kuwa hakuna mwenye uwezo wa kufyeka miti hiyo hadi leo. “Walipoona miti imeota, ikabidi walime barabara kuzunguka msitu wetu, wao waliambiwa wapande miti nje ya msitu huu na sio kuufyeka. Hii ndiyo simulizi ya kwanza ya maajabu ya Nyumbanitu.”

Jana, habari hii ya simulizi ya Msitu wa Nyumbanitu iliisha wakati mmoja wa waongozaji wetu, Alex aliporudia sharti la kutembea kwa mstari na hakutaka kuona watu wakijiachia, akitaka utembeaji uwe wa nidhamu ya hali ya juu. Leo tunapita eneo jingine la ajabu.  Sasa endelea…

Mwongozaji alitutaka tuvue viatu ili kupita eneo hili lenye ardhi laini.

Japo tulivua viatu, ardhi ya Nyumbanitu ni laini kama unatembea juu ya godoro.

Tulitembea bila kuchomwa na miiba wala mabaki ya miti tukielekea katikati ya msitu ambako ndiko makao makuu ya Nyumbanitu. Upepo mkali uliokuwa ukivuma juu ya miti na sauti za ndege ndivyo vinavyosikika wakati huu.

Wakati tukitembea, Julius Msigwa anaendelea kusimulia mambo tofauti na anasema watu huingia kwenye msitu huu kwa nia tofauti.

Anasema wapo wanaoingia kwa nia ya kufanya matambiko, kujifunza, kutalii, kuchuma dawa kwa madai kuwa kila aina ya jani la miti yam situ huu hutumika kutibu ugonjwa fulani.

Miongoni mwa wageni waliotembelea msitu siku hii ni Dk Peter Kiliwo, ambaye ni kiongozi wa timu ya uzinduzi wa Mradi wa Kuimarisha Mfumo wa Sekta za Umma (PS3). Dk Kiliwo anasema hakuwahi kuusikia simulizi za msitu huo kabla.

“Ni msitu wa ajabu ambao ungetangazwa Watanzania tungeujua siku nyingi. Ardhi hii nyororo inanishangaza na sijawahi kusikia habari za msitu huu kabla,” anasema Dk Kiliwo huku safari ya kuelekea katikati ya msituni ikiendelea.

Katikati ya msitu

Hatimaye tulifika katikati ya msitu. Eneo hili linatisha kuliko kawaida kwa kuwa ndilo ambalo hutumiwa na wenyeji kwa ajili ya matambiko.

“Hapa ndipo kuna kila kitu cha kimila ambacho Wabena hutumia kwenye ibada zao za jadi.

“Eneo hili tunatumia kwa ajili ya ibada na nitapatumia kuwasimulia historia ya msitu huu,” anasema Julius.

Kila mmoja anatulia kumsikiliza akitoa  maelezo. Hakuna aliyeusogelea mti umevishwa nguo nyeusi na kufungwa mnedzi, kitu chenye manyoya marefu ya kuchanua yaliyo na rangi nyeusi mithili ya mkia wa farasi.

Mti huo umezungukwa na zana nyingine kama kigoda, mkuki na ungo uliosheheni tunguli ambazo wenyewe hutumia kuwasaidia wale wenye nia ya kupata tiba.

Julius anakaa kwenye kigoda tayari kutoa simulizi ya msitu huo. Kabla hajaanza, ghafla tawi la mti lililokauka linaanguka karibu na eneo tulipo.

Jambo hili linasababisha tafrani na baadhi kutaka kutimua mbio.

“Msiogope, wazee walishawapokea huu ni mti tu, kuweni na amani,” anasema Julius.

Simulizi ya msitu

Julius anasema huo ndiyo msitu wa asili wa kabila la Wabena wanaopatikana wilaya za Njombe na Wanging’ombe mkoani Njombe.

Msitu huo ni wa asili na ulitunzwa tangu enzi za mababu.

Anasema inasemekana kuwa Nyumbanitu ulianza kuwa maarufu baada ya Chifu wa wabena, Mkongwa kuwaita wanae watatu na kuwakabidhi majukumu kulingana na uwezo wa kila mmoja.

“Chifu alisoma tabia za watoto wake na kwa sababu alitaka kuuendeleza Ubena, ilibidi awakabidhi madaraka watoto wake,” anasema.

“Mtoto wa kwanza aliitwa Fute. Huyu alipewa jembe kama ishara ya kuwa mkulima hodari, akitakiwa kuhakikisha anasimamia shughuli za kilimo ili kuepuka janga la njaa.”

Anasema mtoto wa wapili aliyeitwa Mkongwa alikabidhiwa mkuki kwa ishara ya kupewa ruhusa ya kupambana na maadui, huku akipewa kazi ya utawala.

“Kama utakumbuka historia, machifu wa makabila walipigana na hapo ndipo sisi na Wangoni tulipotengeneza utani. Huyu Mkongwa alikuwa shujaa wa vita,” anasisitiza.

“Mtoto wa mwisho alikabidhiwa ungo kwa maana ya kuwa mganga wa jadi.  Huyu ndiye aliyepewa jukumu la kufanya matambiko na kuongoza vikao vyote vya kimila.”

Julius anasema mtoto huyo ndiye alipewa kazi ya kuulinda na kuutunza msitu huo.

Anasema kazi zote hizo zilifanyika kwenye msitu huo na zana zote walizokabidhiwa watoto hao zimehifadhiwa ndani ya msitu huo hadi leo na ndizo tulizokuwa tukionyeshwa.

Kuku weusi

Kama tulivyoelezwa awali, kwenye msitu huu kuna kuku wa ajabu. Julius anasema hakuna anayejua kuku wanaoishi kwenye msitu huu waliingiaje.

Anasema kuku hao huonekana zaidi wakati wa mavuno, yaani kiangazi na inapofika msimu wa mvua ni nadra kukutana nao.

Wananchi wa Kijiji cha Mlevela wanasema kuku wa Nyumbanitu, hata ikitokea wameingia kijijini, hakuna anayewakamata kwa kuwaogopa.

Hata hivyo, Julius anasema kuna mtu mmoja anayejishughulisha na biashara ya kuku, aliamua kuwakamata kuku hao alipowaona wakila wadudu kando ya barabara karibu na msitu huo. Alikuwa anataka kuwauza.

 “Yule jamaa aliwachanganya na kuku wengine na kwenda nao hadi mjini akawauze na wengine wote, lakini huyu hakuuzika. Kila mtu alikataa kumchukua,” anasema.

Anasema ilipofika jioni alianza safari ya kurejea kijijini, lakini ilikuwa vigumu kusukuma baiskeli iliyokuwa na kuku huyo kutokana na uzito wake.

“Kilichomshangaza kwamba kuku yule si wa kawaida kutokana baiskeli kuwa nzito. Aliisukuma kwa shida hadi alipofika karibu na msitu ambako baiskeli ilianguka, tenga likavunjika na kuku akakimbilia msituni,” anasema.

Anasema mfanyabiashara huyo alianza kupiga kelele kuomba msaada, kwa kuwa wakati huo wote alihisi kubeba mzigo mzito. Watunzaji wa msitu walipofika, walimtaka aombe msamaha kwa kitendo chake cha wizi alichotaka kukifanya, vinginevyo angedhurika.

Japo sikubahatika kukutana na mfanyabiashara huyo, mkazi wa Kijiji cha Mlevela, Lukas Mkongwa anasema wakibaini kuwa mnyama yoyote anatokea kwenye Msitu wa Nyumbanitu, huwa hawahangaiki naye.

Julius anasimulia mkasa mwingine unamhusu dereva wa gari aliyegonga kuku wakati akivuka barabara.

“Yule dereva alipogonga aliendelea na safari, lakini mbele kidogo gari yake ikapata shida. Wenyeji wakamshauri arejee msituni kuomba radhi. Alipofanya hivyo, safari yake iliendelea,” anasema.

Kuku wa msitu huo ni wapole, weusi wenye mdomo mwekundu ambao wakitoka nje ya msitu, mtu anaweza kudhani wa kufugwa.

Kikubwa ni kwamba kuku hao hawaliwi kama ilivyo kwa kuku wa kawaida.

Wanyama kama ng’ombe, mbuzi na kondoo wanaoingia kwenye msitu huo huwa na rangi nyeusi.

Upo msimu ambao ng’ombe wa ajabu huonekana kwenye msitu huu.

“Wengi hawajabahatika kuona ng’ombe hao ambao hujichunga wenyewe, lakini huja kwenye msitu wetu kwa nadra na ikitokea hivyo, lazima kuna jambo kubwa,” anasema Julius tukiwa katikati ya msitu.

Hata hivyo, anaeleza kuwa miaka ya zamani, makundi ya ng’ombe weusi walikuwa wakiingia kwenye msitu huu mara kwa mara, lakini hali sasa imebadilika.

Walokole waingia msituni kuomba

Julius pia anasema simulizi za ajabu za msitu huu na kuwapo kwa imani za kishirikina, ziliwafanya baadhi ya waumini wa Kikristo wanaojulikana kama walokole vijiji vya jirani kuamua kuingia ili kufanya maombi.

“Hili si tukio la siku nyingi, hawa watu walitaka kuja kukemea mashetani ndani ya msitu,” anasema.

“Siku ya maombi yao, walokole hao walijikusanya na kuanza safari hadi msituni. Walipofika waliamua kuingia bila kukutana na mwenyeji yoyote wala kufuata mila na desturi za kuingia msituni ili kutoka salama.

“Walikuja moja kwa moja hadi kwenye mti huu, walianza kukemea na kuvuruga utaratibu wa hivi vifaa vya matambiko,” anasema.

Julius anasema watu hao waliendelea na maombi kwa siku nzima, ilipoisha wakataka kuanza safari ya kutoka ndani ya msitu.

Julius anasema hakukuwa na njia ya kuwawezesha kutoka ndani ya msitu.

“Walijikuta wakiendelea kupiga kelele, wakizunguka msitu mzima lakini hakukuwa na msaada kwa wao kutoka,” anasema.

Watu waliokuwa wakipita nje ya msitu walisikia kelele, hata hivyo hawakuwa na msaada wowote kwani hata wao hawawezi kuingia bila kufuata taratibu.
INAENDELEA KESHO