Mtibwa ijipange vyema, isirudie makosa ya Kombe la Shirikisho Afrika

Monday July 9 2018

 

Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limetoa ruksa kwa timu ya Mtibwa Sugar kushiriki mashindano ya kimataifa, baada ya kutwaa Kombe la Shirikisho.

Mtibwa ilifungiwa miaka mitatu na CAF kushiriki mashindano ya kimataifa, baada ya kugoma kwenda Afrika Kusini kucheza mchezo wa marudiano na klabu ya Santos.

Hata hivyo, Mtibwa itakuwa na sifa ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika endapo italipa faini Dola 1,500 na kulipa fidia ya maandalizi ya mchezo huo kwa klabu ya Santos.

Shirikisho hilo limeipa klabu hiyo ya Manungu, Turiani hadi Julai 20 kulipa faini na fidia hiyo kabla ya kuruhusiwa kushiriki tena mashindano ya kimataifa.

Mtibwa ilitenda kosa hilo mwaka 2004 katika mchezo wa mashindano ya Kombe la CAF baada ya mechi ya awali iliyochezwa nchini, kufungwa mabao 3-0 na Santos.

Mtibwa ilifanya kioja hicho ikiwa ni mara yake ya kwanza kucheza mashindano ya kimataifa ikiamini kwamba haitaweza kusonga mbele katika mchezo wa marudiano uliokuwa umepangwa kuchezwa Jijini Cape Town.

Timu hiyo iliyokuwa ikihitaji ushindi wa mabao 4-0 kuing’oa Santos ilianya uamuzi usiokuwa na tija ambao hadi leo unawatafuna viongozi wa klabu hiyo iliyowahi kupika wachezaji waliokuwa tishio katika klabu za Simba, Yanga na timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’.

Huwezi kutaja mafanikio ya Mtibwa bila kuwataja nyota waliowika akina Salhina Mjengwa, John Thomas ‘Masamaki’, Kassim Mwabuda, Abubakari Mkangwa, Monja Liseki, Kassim Issa, Geofrey Magori na Mecky Mexime waliotikisa anga la soka enzi zao.

Bila shaka kitendo cha kufungiwa miaka mitatu kilichangia kwa kiasi kikubwa Mtibwa kupoteza dira ya ushindani hasa katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Baada ya kupoteza kizazi cha kina Mkangwa, Mtibwa ilianza kusajili wachezaji wa kawaida kwa kisingizio kuwa hata wakifanya vizuri katika ligi hawatashiriki mashindano ya kimataifa.

Hata hivyo, ilizinduka msimu uliopita kwa kuonyesha dhamira ya kushiriki mashindano ya kimataifa, baada ya kucheza vyema mechi za Kombe la Shirikisho ikiwamo kuilaza Singida United mabao 3-2 katika mchezo wa fainali.

Mtibwa inastahili pongezi kwa kuonyesha dhamira ya dhati ya kuwania nafasi hiyo kwa kuwa licha ya kuwa ‘kifungoni’ ilicheza kwa kujituma katika mechi zake zote ikiwemo ya fainali kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Mafanikio ya Mtibwa yametokana na ushirikiano baina ya viongozi, wachezaji, benchi la ufundi na wadau wanaoizunguka klabu hiyo yenye maskani mkoani Morogoro.

Kocha wa timu hiyo Shabani Katwila alionyesha ukomavu tangu kwa mwanzo timu hiyo ilipoanza kampeni ya kuwania ubingwa kwa kuwahimiza wachezaji kucheza kufa au kupona ili kukata tiketi kucheza mashindano ya kimataifa.

Licha ya kupata nafasi ya kucheza mashindano ya kimataifa, Mtibwa ina wajibu wa kufanya maandalizi kabambe kwa kuwa inakwenda kushindana na timu zenye viwango bora.

Mtibwa itambue inakwenda kushindana na timu zilizofanya maandalizi ya kutosha katika eneo la kiufundi, hivyo haiwezi kukwepa kujiandaa kikamilifu katika nyanja zote kama inahitaji kupata ushindi.

Timu hiyo inakwenda kukutana na vigogo wa soka Afrika ambao wana uzoefu wa kutosha katika mashindano ya kimataifa, hivyo ina wajibu wa kufanya usajili makini kwa kuzingatia mahitaji ya benchi la ufundi.

Mabingwa hao mara mbili wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1999 na 2000 wana nafasi nzuri ya kujenga timu imara kwa kuwa benchi la ufundi limeona kasoro zilizojitokeza kwenye mashindano hayo msimu uliopita.

Bila shaka kocha Zuberi Katwila amekabidhi kwa viongozi ripoti ya mashindano hayo na moja ya eneo ambalo anataka kufanyia kazi ni kujenga timu imara ya ushindani kwa kusajili wachezaji bora wenye uzoefu wa mechi za kimataifa.

Ingawa timu hiyo inaundwa na wachezaji waliodumu muda mrefu, bado inatakiwa kupata nyota wapya ambao watakuwa chachu ya kuiletea mafanikio katika mashindano ya kimataifa.

Kimsingi Mtibwa sio timu ya ngeni katika mashindano ya kimataifa, viongozi wake uelewa mpana wa kuchagua njia sahihi ya kupita ili kuipa mafanikio timu hiyo ambayo imekuwa tishio katika ligi ya ndani.

Naamini Mtibwa imejifunza kutokana na kosa la mwaka 2004, hivyo itakuwa makini katika maandalizi ya mashindano ya kimataifa.

Nafasi iliyopata ni adhimu, hivyo inapaswa kuitumia kwa kuwa wawakilishi wazuri wa Tanzania Bara kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.