Mtoto pia anaweza akiwezeshwa

Muktasari:

Kadiri mtoto anavyokua, ndivyo anavyokutana na mambo ambayo yanaganda kwenye akili yake. Kwa mfano akiwa katika familia yenye upendo na amani ni wazi kuwa ndivyo atakavyoishi kipindi akiwa mtu mzima anayejitegemea.

Maisha ya kila siku yanabeba mambo mengi sana. Kuna majaribu, mafanikio, changamoto, chuki, mapenzi na kadhalika. Mambo haya tumezowea kusema kuwa kila mmoja anaumbwa na ya kwake, lakini kuna kila ushahidi kuwa mambo yote yanayofanyika ukubwani huandaliwa kutokea utotoni.

Kadiri mtoto anavyokua, ndivyo anavyokutana na mambo ambayo yanaganda kwenye akili yake. Kwa mfano akiwa katika familia yenye upendo na amani ni wazi kuwa ndivyo atakavyoishi kipindi akiwa mtu mzima anayejitegemea.

Lakini akiishi kwenye familia yenye chuki na visasi basi kadhalika naye ukubwani atakuwa mtu wa aina hiyo. Hata kama atahudumu kama mtumishi wa Mungu, akiwa na roho ya kishetani basi ni shetani tu. Wa kale walisema huwezi kukielewa kitabu kwa kuangalia jalada lake tu. Ndivyo isivyowezekana kutambua undani wa mtu kwa kumtazama muonekano wake wa nje.

Hii inamaanisha kuwa unaweza kumpa daraja za juu mtu anayevaa suti na kutembelea gari za kifahari zaidi ya mvaaji wa mitumba anayeendesha baiskeli. Lakini unaweza kukuta huyu mvaa suti ni jambazi na muuaji mkubwa wakati mwendesha baiskeli akawa mchunga kondoo wa Bwana.

Mashirika mengi ya Kimataifa yamegundua kuwa mtoto anayepewa mbinu za kuendeleza kipaji chake ana uwezo wa kufanya vizuri zaidi maishani. Mashirika haya yamekuwa yakifanya uwek

ezaji kwenye nchi masikini kwa kuanzia na watoto. Mfano hai ni jinsi Wamarekani walivyojikita kwenye soka la watoto nchini Brazil.

Uzuri wa mtoto ni uwezo wake wa kujifunza kwa asilimia zote. Anapokea kama anavyofundishwa. Bila shaka ni kwa sababu hana mambo yanayoweza kumtinga na kumharibia umakini. Ni tofauti na kumfundisha mtu mzima mwenye familia, anaweza kuvurugwa na matatizo ya nyumbani.

Hakuna nchi duniani inayofanya vizuri kwenye medani zote zikiwemo siasa, uchumi, elimu, biashara, burudani na michezo bila kuwekeza kwa watoto. Wengine wanafanikiwa bila kujua kuwa walitoa nafasi kwa watoto. Lakini ukweli unabaki pale pale.

Unaweza kushangaa siasa inahusianaje na watoto. Lakini ukitazama Mataifa ya Uchina na Israel utagundua kuwa kule siasa ni maisha yanayomhusu kila mmoja; mtoto, kijana hadi mzee. Watoto walifunzwa uzalendo kupitia siasa na kuitikia mwito wa kila mmoja kuwa mlinzi wa Taifa lake.

Yapo mambo kadhaa tuliyoyafuata kutoka huko kama Chipukizi na JKT. Hakuna anayeweza kupita kwenye njia za maisha bila kufundwa na asasi hizo. Na hakuna anayepinga kuwa uzalendo na maadili ya wakati ule yametofautiana kwa kiasi kikubwa na jinsi ilivyo sasa.

Mambo haya yaliweza kumjenga mtoto kwenye misimamo thabiti juu ya Utaifa wake. Na ilisaidia kumfanya mtoto huyo kuwa mzalendo aliyelaani rushwa na kupingana na ufisadi na matumizi mabaya ya mali ya umma.

Kama nilivyosema awali, Mataifa tajiri kama Marekani yamewekeza mitaji mikubwa kwenye vyuo, viwanda na taasisi za burudani na michezo ya watoto yakiwa na uhakika wa kuvuna yalichopanda. Lakini si kwamba mataifa hayo yaliota au kubahatisha, bali yaliona utashi wa masikini hao.

Ikumbukwe kuwa nyota wa Brazil na dunia, Ronaldinho aliibuliwa akiwa kwenye mpira wa chandimu hadi kuwa nembo ya soka duniani. Wamarekani wamefanya uwekezaji mkubwa kiasi cha kuipandisha thamani michezo hiyo hadi kuweza kujiendesha kwa faida.

Katika kuonesha uwezo wa watoto kama wakiwezeshwa, tumeona jinsi watoto waishio kwenye mazingira magumu walivyoweza kuchukua Kombe la Dunia mwaka 2014 katika mashindano yaliyozishirikisha timu za mataifa mbalimbali duniani huko Rio de Janeiro, Brazil.

Ikiwa imetinga fainali za Kombe la Dunia kwa watoto wa mitaani kwa mara ya pili mfululizo, timu hiyo ya Tanzania iliweza kutwaa kombe hilo linalojulikana kama Street Child World Cup.

Timu ilionesha kiwango cha juu hata kuzishinda timu ngumu kama Burundi, Marekani, Indonesia, Nicaragua, Ufilipino na Argentina. Golikipa wa Tanzania Emmanuel aliweza kuchaguliwa kuwa golikipa bora wa michuano hiyo inayotambuliwa na Shirikisho la Soka Duniani, FIFA.

Katika hali kama ile, hakuna mwekezaji ambaye angeweza kusita kuingiza fungu kuendeleza soka la watoto wa mtaani. Lakini kwa kukosa mipango ya kueleweka, timu hiyo haikutafutiwa wawekezaji wala kufanyiwa matangazo yaliyostahili, na hadithi ikaishia hapo.

Pengine ni kukosa malengo maalum ndiko kunakotufanya tushindwe kuendeleza mazuri kama haya. Hatuamini kama watoto wetu wanaweza, bali tunaichukulia kuwa bahati. Ilisemwa kuwa kijacho bila mipango huondoka bila mipango, na ndio maana hatuoni muendelezo.

Si ajabu Kombe la Dunia lilikuwa moja kati ya tuzo tulizostahili kutokana na vipaji tulivyo navyo.

Lakini si ajabu pia hali kama hiyo ingetokea kama tungeamua kuwaendeleza watoto kwenye michezo ya riadha, ndondi, kikapu, meza, wavu na mingineyo. Tungepata heshima na makombe mengine lukuki.