Mwasiti ana siri nzito kuhusu mapenzi

Saturday January 23 2016Mwasiti

Mwasiti 

By Herieth Makwetta, Mwananchi

Wakati tabia ya mastaa wanaochipukia ya kuwaanika wapenzi wao kwenye mitandao ya kijamii ikishamiri, msanii Mwasiti Almasi amesema hataweza kumtangaza mchumba wake hata iweje.

Mwasiti ambaye kwa kipindi chote cha ustaa wake hajawahi kusikika akimtaja mpenzi wake yeyote hadharani, ametoa masharti mawili kwa mashabiki wake na jamii ili kumjua mpenzi wake huyo.

Msanii huyo anayetamba na wimbo ‘Sema nae’ aliomshirikisha Queen Darlin, ameliambia Starehe kuwa, waliotega masikio kumjua mpenzi wake, wasubiri siku atakapofunga pingu za maisha.

Mwasiti anasema kwa kipindi kirefu amekuwa akishindwa kutangaza uhusiano wake wa kimapenzi kwa kuhofia kuchafuliwa jina lake, lakini kubwa zaidi hajawahi kuanzisha urafiki na wanaume wengi kama ilivyo kwa wasichana wengine.

Alisema akiwa binti, anahofia pia kutangaza uhusiano kabla ya ndoa kwa kuwa unaweza usidumu na badala yake akawa na mpenzi mwingine jambo litakalomtafsiri vibaya mbele ya jamii inayomwamini na kumfuata kama mfano wa kuigwa.

“Uhusiano wa kimapenzi utabaki kuwa wa Mwasiti, lakini nyimbo ni zetu sote. Mpaka nitakapokufa au nitakapofunga ndoa ndipo watu watamjua mpenzi wangu ni nani. Mimi ni binadamu kama walivyo wengine, nitakuwa tayari kumtangaza mwenyewe nitakapofunga ndoa au la,” alisema kwa msisitizo.

Alipoulizwa uhusiano kuhusu nyimbo anazoimba zinazoonyesha dhahiri kutendwa kimapenzi, iwapo zinalandana na uhusiano wake, Mwasiti anafafanua kuwa nyimbo za aina hiyo ni sehemu ya kazi yake.

Anasema kwake yeye alichagua kuimba aina hiyo ya muziki ili kuisemea jamii kubwa ambayo inatendwa na mapenzi.

“Ukiangalia Celine Dion anaongelea mapenzi. Nilichagua mapenzi kwani yanamgusa baba na mtoto, ndugu jamaa na marafiki.. Niliamua kuimba upande wa watu wanaoumizwa lakini haimaanishi kwamba nilitendwa au ninatendwa katika mapenzi,” anasema Mwasiti.

 

2016 mwaka wa kazi

Akiwa ameufungua mwaka kwa wimbo ‘Sema nae’, Mwasiti anasema huu ni mwaka wake wa kazi kwani amejipanga kuhakikisha anakamilisha albamu yake na kusambaza nyimbo tatu.

Kwa mujibu wa Mwasiti, atahakikisha kuwa mashabiki wake wanapata kile walichokikosa kwake kwa muda mrefu baada ya kuwa pembeni kwa muda.

Mwasiti anasema mwaka 2015 ulikuwa ni mwaka ambao hakufanya kazi kikamilifu, kiasi kwamba amelaumiwa na mashabiki wake.

Anasema kwa sasa amejipanga kutoa wimbo siku ya Valentine aliomshirikisha Barnaba.

“Nitatoa nyimbo lakini nitaendelea kurekodi hapa nchini na hata video zangu nitafanya Tanzania. Kutengeneza video Afrika Kusini siyo fasheni, kabla hujaamua kufanya hivyo ni vyema kuhakikisha kwamba soko lako la ndani zuri na huko nje uwe na uhakika kwamba fedha yako itarudi na soko lako zuri pia,” anasema msanii huyo ambaye mwanzo wa ke wa kujulikana ni baada ya kibuka na wimbo ‘Niambie’.