MAONI: Nanenane isiishie kwenye maonyesho

Friday August 9 2019

Wakulima na wafugaji wa Tanzania jana waliadhimisha Sikukuu ya Nanenane ambayo aghalabu hutoa fursa kwao, taasisi na wadau mbalimbali wa kilimo nchini kuonyesha mafanikio na ubunifu mbalimbali katika sekta hiyo.

Awali, Nanenane ilikuwa ikiadhimishwa kila Jula 7 ikiitwa Sikukuu ya Sabasaba kabla ya kuhamishiwa Agosti 8 na siku hiyo ya asili ikibaki kuwa mahsusi kwa maonyesho ya biashara. Mwaka 1977, Sabasaba ilipoanza kuadhimishwa ililenga kuongezea nguvu sera ya Serikali wakati huo ya Siasa ni Kilimo ambako wakulima katika kila pembe ya nchi walionyesha mafanikio waliyopata kwa maana ya mazao yao huku wadau wengine wakionyesha pembejeo na maofisa ugani kutoa elimu mbalimbali alimradi lengo lilikuwa ni kuongeza tija katika kilimo.

Tangu wakati huo, malengo yamekuwa hayohayo, yakiboreshwa ili kukidhi mahitaji ya wakati na mabadiliko ya kiteknolojia.

Mbali ya maonyesho hayo kutumika kuonyesha mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo na kubadilishana ujuzi na mbinu za kuboresha shughuli zao, wakulima na wadau wamekuwa wakiyatumia kufanya tathmini ya hali ya kilimo.

Kila mwaka katika siku hii, viongozi mbalimbali hasa wa kitaifa wamekuwa wakitoa ujumbe kwa wakulima na watumishi wa umma wanaohusika na sekta hiyo kuongeza bidii kufanikisha kilimo ambacho ndicho kilichoajiri idadi kubwa zaidi ya watu nchini.

Jana, akiwa katika sherehe za kilele cha siku hiyo kwenye viwanja vya maonyesho ya Nyakabindi wilayani Bariadi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaagiza wataalamu wa kilimo, mifugo na uvuvi kutoka Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Magereza kwenda vijijini kwa wakulima kuwafundisha mbinu bora ya kilimo chenye tija.

Advertisement

Pia, aliagiza shughuli zinazofanyika katika bustani na mashamba ya taasisi hizo ziwe za kudumu kuwezesha wakulima kutembelea na kujifunza. Aliwaambia, “Msisubiri hadi wakati wa maonyesho ya Nanenane; mashamba na shughuli hizi (za kilimo) ziwe za kudumu kipindi chote cha mwaka.”

Pia, Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Kilimo kusambaza utaalamu na mashine ya kupima udongo katika kila mkoa na halmashauri nchini kuwezesha wakulima kupima na kujua virutubisho vilivyomo na vinavyokosekana kwenye maeneo yao akisema hiyo itawapunguzia gharama wakulima ya kutumia pembejeo zisizohitajika na itawawezesha kulima kwa tija huku wakifahamu kiwango cha mavuno wanayotarajia.

Akiwa katika kilele cha siku hiyo huko Morogoro jana, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan aliwaagiza watafiti wa kilimo kuendelea kufanya tafiti zitakazotoa suluhisho la kupunguza gharama za kilimo kwa wakulima na hivyo kuongeza tija ya uzalishaji.

Tamaa yetu ni kuona kwamba maonyesho haya hayaishii tu kuonyesha mafanikio yaliyotokana na wakulima walioboresha mashamba yao na teknolojia zilizopo sokoni za kuinua sekta hiyo, bali yanatumika kufanya tathmini ya kina juu ya utekelezaji wa maagizo ya viongozi na wataalamu wa kilimo na mifugo yaliyotolewa katika mwaka uliotangulia. Tunaamini kwamba Nanenane ikizingatiwa vyema, maisha ya wakulima na bila shaka, Watanzania walio wengi yataboreka. Inawezekana kila mmoja akitimiza wajibu wake.