Nguvu iliyotumika kusema mabaya ya Chid Benz, itumike kusema mazuri yake

Muktasari:

Wiki hii tumeona msanii Ferooz ametoa wimbo wake akiwa na G Nako ambapo wimbo huo waitwa ‘Excellent’ ambapo ni wimbo mzuri na wenye ubora wa Ferooz.

Hakuna haja ya kuuma maneno katika kupeana ile kweli yenye kuleta uhuru katika maisha yetu ya muziki wa kizazi kipya. Licha ya uhalisia maisha ya kwenye muziki wa kizazi kipya yamejaa habari mbaya ambazo hazijengi bali kubomoa.

Na uhalisia mwingine ni juu ya mashabiki na wadau ni namna ya kuzungumza mabaya zaidi kwa urefu na ufafanuzi mwema ila ukweli na mambo ya maana kupewa kisogo.

Huku wenyewe wakiamini jambo baya ndiyo husikilizwa vyema, ila uhalisi sio kweli bali watu husikiliza maana hakuna cha kusikiliza.

Jambo hili si jambo jema, na jambo hili limeendelea kuwatumbukiza shimoni wasanii wengi ambao kwa bahati mbaya walipata matatizo tofauti tofauti katika muziki wa kizazi kipya, ilihali uwezo wao kuwa mkubwa katika ufanyaji wa kazi.

Ni kama vile tunafurahia zaidi anguko la wasanii wetu kuliko mafanikio yao. Ndio maana habari mbaya zinapewa kipaumbele katika soga, mitandaoni na hata katika baadhi ya vyombo vya habari.

Wiki hii tumeona msanii Ferooz ametoa wimbo wake akiwa na G Nako ambapo wimbo huo waitwa ‘Excellent’ ambapo ni wimbo mzuri na wenye ubora wa Ferooz.

Lakini ni wapi umeona kwa upana mashabiki na wadau wakimzungumzia kwa ukubwa?

Lakini ingekuwa ni habari mbaya yenye fedheha hakika mashabiki wangeishikilia kiasi kila mmoja kujua fedheha hiyo.

Ni kwamba mashabiki wanapenda zaidi habari zenye fedheha zaidi ama?

Lakini nyakati fulani za nyuma kejeli na dhihaka zilitawala mno juu ya msanii wa hiphop Chid Benz. Kila mtu alisema lake, walioandika kila mtu aliandika lake, lakini pia wapo wasanii kama Q Chief na Kalapina walipewa mahojiano na vyombo vya habari na waliongea mno na kuelezea mabaya yake juu ya matumizi ya dawa za kulevya.

Lakini katika upande wa mashabiki hasa kwenye mitandao ya kijamii kejeli na dhihaka zilitawala.

Ni kama vile jamii haitaki kuona watu wakikiri makosa yao huku wakipewa moyo waweze kusimama tena

Na watu walifanya mambo haya kwa nguvu kubwa mno kiasi kila mmoja alijua. Ni kweli habari mbaya huenea kwa haraka zaidi lakini sisi tumezidisha nguvu huko. Inawezekana kama yangekuwa mashindano, Tanzania tungeibuka kidedea.

Maana yangu kuu ya kunena kejeli na dhihaka ni namna ya watu hawa walivyokuwa wakitumia nguvu na muda kusambaza video za Chid Benz akiwa katika hali isiyofaa, ila sikuona maana ya kusambaza video hizo.

Hakika hakukuwa na maana wala msaada kwa upande wa Chid Benz katika usambazaji wa video zile katika nyakati badala yake ilizidisha tatizo ila kwa mhusika kwa namna ya kujiona hafai tena mbele ya jamii.

Ila jamii inapaswa ijue “Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo” tuna kila sababu ya kuishi katika methali na semi hizi za mswahili maana hutupa ufumbuzi na uthamini wa mambo mengi.

Chid Benz alianguka na sasa ameamka tena na nguvu mpya. Ziim Ziima ni wimbo wake ambao unaonyesha namna gani ameamua kurudi kwenye uwanja wa muziki wa kizazi kipya baada ya kupitia kipindi kigumu.

Hakika yatupasa tumpongeze maana mapito yake ni yenye ugumu zaidi na kuweza kurejea walau na wimbo huu si jambo dogo.

Hakuna kingine anachotakiwa kupewa Chid Benz zaidi ya nafasi tena katika vyombo vya habari na mashabiki.

Chid Benz anahitaji nguvu kubwa ambayo itaweza kumfanya ajisikie faraja kama bado ni msanii mwenye kuthaminika.

Ila kasumba ya mashabiki wengi ni kuvipa nguvu vitu ambavyo havina maana wala faida bali fedheha.

Tazama jinsi mitaa ilivyo kimya juu ya Chid Benz katika wimbo wake wa Ziim Ziima.

Lakini kama ingelikuwa ni jambo lenye soni juu ya Chid Benz hakika ingekuwa ni zungumzo la nyakati nyingi zaidi. Ni vyema ile nguvu iliyotumika kuzungumza mabaya ya Chid Benz itumike tena kuzungumza mazuri yake ya sasa.

Tuwe jamii inayopenda kutangaza mema ya watu na siyo mabaya pekee. Wapo wengi walikengeuka na baadaye kufanya mema lakini hatufanyi juhudi kuyatangaza.

Wasanii hawa wanapofanya kazi wasaidiwe ili wasirudi walipotoka. Kuwatenga, kuwadhihaki kuna tengeneza janga si lao peke yao bali Taifa kwa ujumla.

Mwandishi Bartholomew Bernard Mbulinyingi ni mchambuzi wa masuala ya burudani. Anapatikana kwa simu O719476068

Instagram @iambatro, Twitter @iambatro