HOJA YANGU : Nguvu ya dola haitatatua mkwamo wa kisiasa Z’bar

Sunday May 29 2016Peter Saramba

Peter Saramba 

Ingawa uchaguzi umekwisha, lakini hali siyo shwari katika Visiwa vya karafuu, Zanzibar.

Kuna joto lililosababishwa na mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka jana na ule wa marudio wa Machi 20, mwaka huu.

Zipo sababu nyingi za joto la kisiasa visiwani Zanzibar, lakini kubwa ni uamuzi wa kufuta matokeo ya urais na uwakilishi uliotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar(ZEC), Jecha Salim Jecha.

Pamoja na sababu kadhaa, Jecha alitaja ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ikiwemo kitendo cha mmoja wa wagombea kujitangazia ushindi, jukumu alilodai ni la ZEC.

Uamuzi na tangazo la Jecha lilipingwa na makundi kadhaa kuanzia vyama vya siasa vya ushindani na wadau wengine wa uchaguzi isipokuwa chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM).

Katika tangazo lake, Jecha alisema uchaguzi ungerudiwa ndani ya siku 90, ingawa hilo halikufanyika kwa sababu ambazo hakuna kiongozi yeyote akiwamo Jecha mwenyewe aliyelitolea ufafanuzi.

Baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya kutafuta mwafaka uliohusisha wadau wakuu wa siasa za Zanzibar, CCM na Chama cha Wananchi (CUF), Jecha tena akaibuka na kutangaza Machi 20, mwaka huu, kuwa siku ya uchaguzi wa marudio.

Tangazo hilo lililopingwa kwa nguvu zote na CUF iliyotangaza kuususia uchaguzi huo, ukafurahiwa na CCM ambayo inaaminika ilipoteza uchaguzi ambao matokeo yake yalifutwa na ZEC.

Nimelazimika kuelezea japo kwa ufupi kilichotokea Zanzibar wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita na ule wa marudio ili nipate fursa ya kuelezea yanayotokea visiwani humo hivi sasa.

Kwa wenye kufuatilia siasa za Zanzibar, hali inayoanza kujitokeza sasa inaweza kufananishwa na iliyokuwapo miaka ya awali ya mfumo na uchaguzi wa vyama vingi vya siasa, miaka ile ya 1995 na kuendelea.

Wakati huo, vyama shindani vya kisiasa CCM na CUF vilitoshana nguvu kwenye uchaguzi huku chama tawala kikiibuka na ushindi mwembamba kuanzia kwenye nafasi ya urais kupitia kwa Rais wa wakati huo, Dk Salmin Amour hadi kwenye viti vya uwakilishi na ubunge.

Vyama hivyo viwili viligawana visiwa kwa CCM kutamba Unguja na CUF Pemba.

Kama ilivyo sasa, CUF kupitia kwa mgombea urais wake, Seif Sharif Hamad kilidai kuwa mtokeo halisi yalitafutwa na ZEC kukibeba CCM.

Uhasama wa kisiasa ukaibuka kati ya vyama hivyo na wafuasi wake kiasi cha kufikia hatua ya familia kutengana kutokana na tofauti za kiitikadi.

Taarifa za wana ndoa kupeana talaka kutokana mvutano wa kiitikadi zikawa jambo la kawaida visiwani Zanzibar.

Hali ilikuwa mbaya kiasi cha mali, taasisi na maeneo ya umma ikiwamo visima vya maji kuanza kuhujumiwa kwa kuharibiwa na wakati mwingine kutiwa kinyesi cha binadamu.

Wazanzibari wakaanza kutengana hadi kwenye masuala ya msingi ikiwamo kununua na kuuzia bidhaa.

Jambo baya kuliko yote, ndugu zetu hawa wakafikia hata kususiana au kutengana kwenye misiba ambapo itikadi ya mfiwa au aliyefariki dunia ikageuzwa kigezo cha kuhudhuria au kutohudhuria msiba.

Kwa waliosahau, huko ndiko Zanzibar ilikofikia wakati huo wa awamu ya Komandoo, Dk Salmin hadi awamu ya kwanza ya Rais mstaafu, Abeid Amani Karume.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa msaada wa Serikali ya Muungano ilitumia mbinu na nguvu zote za dola kudhibiti hali, lakini haikuwezekana kudhibiti hisia za watu mioyoni mwao.

Hali ya utangamano, ushirikiano, maelewano au kufahamiana kama wao Wazanzibari wanavyotamka ilirejea baada ya mwafaka wa 2010 uliofikiwa kati ya CCM kupitia kwa Rais Karume na CUF kupitia kwa Maalim Seif.

Mwafaka huo ndiyo chimbuko la Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), uliosababisha wafuasi wa CCM na CUF kujumuika pamoja kusherehekea maadhimisho ya sikukuu za kKitaifa kila mmoja akipeperusha bendera ya chama chake na ile ya Taifa bila kukwaruzana.

Hata hivyo, Zanzibar ya sasa inaelekea kurejea kwenye uhasama ule wa miaka ya 1990 hadi 2, 000.

Vyombo vya dola pia vimeanza kurejea kwenye mkumbo ule wa miaka ya nyuma kwa kuanza kuwaandama viongozi wa CUF kwa kuwakamata na kuwahoji kutokana na masuala au kauli ambazo kiuhalisia ni za kisiasa zinazostahili kujibiwa na wanasiasa.

Orodha ya viongozi wa CUF ambao aidha wamekatawa au kuitwa na kuhojiwa na polisi ni ndefu, lakini itoshe tu kumtaja Maalim Seif ambaye aliitwa kwa ajili ya mahojiano Ijumaa ya Mei 27, mwaka huu.

Ingawa ni jukumu la Polisi kuhakikisha ulinzi, usalama na utii wa sheria nchini ni vema watendaji wa jeshi hilo wakajiepusha na mihemko ya kisiasa kwa kufanya kazi kwa msukumo au kwa lengo la kuwafurahisha wanasiasa walioshika hatamu ya uongozi.

Nionavyo mimi, mkwamo wa kisiasa Zanzibar hauwezi na kamwe hautatatuliwa kwa matumizi ya vyombo vya dola, bali mazungumzo yenye nia ya dhati miongoni mwa wanasiasa na viongozi wa CCM na CUF, kote Bara na visiwani. Mungu ibariki Tanzania! [email protected], 0766434354.-