UCHAMBUZI: Nida isiwe kikwazo cha urasimishaji wa biashara

Hivi karibuni baadhi ya wakazi wa Kanda ya Ziwa walipongeza juhudi za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), kwa kuwarahisishia usajili kwa njia ya mtandao, na hivyo kuwapunguzia gharama na usumbufu wa safari.

Baadhi ya vituo vya televisheni viliwaonyesha wananchi walioshiriki mafunzo wakipongeza hatua hiyo, wakisema kwamba wamehakikishiwa sasa wanaweza kusajili majina ya biashara zao hata wakiwa vyumbani mwao kwa kutuma taarifa zao kupitia mtandaoni.

Kauli za wananchi hao zilikuwa zinaamsha ari kwa wengine kurasimisha biashara zao kupitia mfumo rasmi wa Brela, ili nao watambulike kama walipa kodi ambao kwa upande wa pili wana haki ya kunufaika na fursa zinazotolewa na Serikali.

Hata hivyo, furaha ya wananchi hao inaweza kutiwa doa watakapoanza usajili wa biashara zao kwa vitendo kwa njia ya mtandao.

Kuanzia hapo wataanzia kukutana na vikwazo ambavyo pengine havikutajwa wakati wa mafunzo yao.

Kwa vyovyote vile usajili wa kile walichokuwa wanakifurahia hauwezi kukamilika wakiwa vyumbani mwao bila kuwa na kitambulisho kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida)na maombi mengi yamekwama kwa sababu hiyo.

Kwa kuwa si wananchi wote waliopata vitambulisho vya Taifa mpaka sasa, mwananchi anayetaka kusajili jina la biashara kupitia mtandao wa Brela hawezi kufanya lolote la maana mpaka atakapokuwa na kitambulisho hicho.

Pamoja na kuwa katika ofisi za Nida ngazi za wilaya maombi ya kitambulisho kwa ajili ya mchakato wa usajili wa biashara na pasipoti unadaiwa kupewa kipaumbele, kiuhalisia jambo hili linachukuliwa kwa wepesi sana na halipo kama inavyosemwa.

Mathalani ni zaidi ya miezi miwili sasa tangu mmoja wa wananchi kupitia ofisi za Nida Manispaa ya Bukoba alipotuma ombi la kupatiwa kitambulisho ili aweze kuendelea na mchakato wa usajili wa jina la biashara kupitia mtandao wa Brela.

Majibu ya muda wote kutoka katika ofisi hii ni kuwa namba ya kitambulisho inaonekana kwenye mtandao na atajulishwa kitambulisho chake kitakapofika. Mtu huyu huenda akasubiri mpaka mwakani bila kurasimisha biashara yake.

Ni njia ambayo inaikosesha Serikali mapato kwa kuweka vikwazo vinavyowakatisha tamaa wananchi washindwe kusajili majina ya biashara na kutambulika rasmi.

Ni njia inayodhoofisha jitihada za kuongeza idadi ya biashara zilizosajiliwa.

Utaratibu wa Nida si rafiki kwa wananchi wanaotaka kurasimisha biashara zao kama ambavyo tovuti ya mamlaka hiyo (www.nida.go.tz) ilivyobeba namba za simu ambazo wakati mwingine hazipatikani hewani.

Hata barua pepe zinazotumwa kupitia anwani ya [email protected] iliyopo kwenye tovuti ya mamlaka hazijibiwi, jambo linaloibua hisia za kutojali malalamiko na maoni ya wanaotafuta ufumbuzi wa changamoto za kukosa kitambulisho.

Hii ni tovuti muhimu na haingii akilini kuona muda mwingi mawasiliano yaliyowekwa humo hayapatikani. Naomba nitaje namba zilizomo ambazo kuzipata ni muhali. Namba hizo ni: 0765201020, 0759102010 na 255222664169.

Namba hizi hazipatikani hivyo mwananchi hawezi kupata maelezo ya ziada baada ya kukwama kusajili biashara yake kwa kukosa kitambulisho.

Kwa nyakati tofauti Rais John Magufuli ameonyesha kutoridhishwa na viwango vya ukusanyaji wa mapato ambavyo kwa vyovyote vile ongezeko lazima lichangiwe na wingi wa biashara zinazosajiliwa kupitia Brela huku akikemea viwango vikubwa vya kodi.

Kama hivi ndivyo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) inatakiwa kuboresha mfumo wake ili kukidhi mahitaji ya upatikanaji wa vitambulisho kwa dharura kwa ajili ya usajili wa huduma zinazotolewa kwa njia ya mtandao.

Kinyume chake ni kufanya juhudi za Brela kuhamasisha usajili wa biashara zikose tija, kwa kuwa kikwazo cha ucheleweshaji wa kitambulisho kinakatisha tamaa na kuvunja moyo wananchi wanaotaka kurasimisha shughuli zao.

Urasimu wa kutoa vibali ni chanzo cha kukwama kwa shughuli mbalimbali ikiwemo miradi ya kiuchumi. Iwapo Brela itakuwa na maombi kidogo ya usajili wa majina ya biashara, basi anguko lao linaanzia Nida.

Haiwezekani mwananchi atake kurasimisha biashara yake Brela ili hatimaye awe sehemu ya walipa kodi, lakini jitihada zake zinakwazwa na chombo kingine tena cha Serikali.

Phinias Bashaya ni mwandishi mkoani Kagera: 0767489094