UCHAMBUZI: Nyumba hizi zinalitia doa Jiji la Mwanza

Jiji la Mwanza ni miongoni mwa majiji yanayokua kwa kasi, si tu hapa nchini bali pia katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Jiji hili linaloundwa na halmashauri mbili za Nyamagana na Ilemela, linatajwa kuwa kitovu cha uwekezaji katika nchi za Afrika Mashariki.

Hata hivyo, jiji hili linatiwa doa na kuwapo kwa majengo na nyumba ambazo zimechoka na kuchakaa kiasi cha kutokuwa na hadhi ya kuendelea kuwapo katikati ya jiji hilo.

Nizipongeze idara zinazohusika na usimamizi wa miundombinu ya barabara ambazo kwa sasa zimeanza kuchukua hatua ama ya kujenga, kurekebisha au kufanyia ukarabati wa baadhi ya barabara zake zinazounganisha mitaa hiyo, ambazo zilikuwa zimechoka zimejaa mashimo na nyingine kutimua vumbi.

Kwa upande huo nadhani wanaohusika wanastahili kongole licha ya kwamba bado hawajafanikisha kwa asilimia 100, lakini kwa hatua zinazochukuliwa inaonyesha kuwapo nia ya dhati na kuleta matumaini katika uimarishaji wa miundombinu hiyo.

Sasa kasheshe na adha kubwa ipo upande wa majengo. Kwa kweli majengo mengi katika mitaa mbalimbali yanatia aibu na kuondosha hadhi ya jiji hilo kutokana na uchakavu wake.

Nisemapo yanashusha hadhi ya jiji, ni kweli. Vipo vijumba katikati ya mji kwenye baadhi ya mitaa ambavyo kimsingi havitakiwi kuwapo kwa hali yoyote ile.

Mitaa hiyo ni pamoja na Mtakuja, Patrice Lumumba, Pamba, Kenyatta, Uhuru, Rufiji, Uzinza, Kwame Nkuruma, Daniel Machemba, Sukuma, Ngokozi, Usumau, Tenge, Unguja, Mission, Mkanyeye na Kilombero ambayo kimsingi ndio mitaa inayotengeneza mji huo.

Kwa mtu ambaye ndio anafika kwa mara ya kwanza katika jiji hilo, kama amefika usiku naamini akifikia kwenye baadhi ya mitaa hiyo, akiamka asubuhi anaweza kubisha kama ndilo jiji linalosikika na kusifika maarufu kama Rock City.

Sawa, nakiri kuwapo majengo ambayo yalijengwa miaka ya 70 lakini kimtazamo na kimwonekano bado yapo vizuri na imara, ambayo sina tatizo wala mashaka nayo.

Lakini vipo vijumba ambavyo bado vimeezekwa kwa mabati ya mapipa ambayo yalikatwa na kufanya shughuli hiyo huku vingine vikiezekwa kwa vipande vya mabati yaliyokatwakatwa enzi hizo ambavyo navyo vimechoka kupita maelezo.

Paa nazo zimechoka na nyingine kuta kudondoka huku baadhi zikizibwa kwa mabati na nyingine zikizibwa kwa kupanga tu matofali bila kujengwa. Hii ni aibu

Ukiachilia mbali kuezekwa kwa mabati ya mapipa na madebe, vipo vijumba vingine ambavyo vimejengwa kwa tope hata vile vilivyojengwa kwa matofali yaliyofyatuliwa kienyeji bila kutumia vifaa maalumu ambayo hata hivyo hayakuweza kupita kwenye tanuru kupata baraka za uimara.

Lakini kwa sasa zipo nyumba ambazo huwezi kujua awali ilikuwa imepakwa rangi ya aina gani kutokana na uchakavu wa nyumba hizo.

Hii yote huenda ni kwa sababu ya wamiliki wa majengo hayo kupenda kukaa mjini kwenye mwanga, lakini hawana uwezo wa kuendeleza makazi yao kulingana na hadhi ya Jiji na kubadilika kwa mazingira.

Lakini kama hiyo ndiyo sababu mbona kwenye baadhi ya majengo hayo yapo yanayotumika kuendeshea biashara, na pengine kutokana na kodi zinazolipwa zingeweza kufanya maendeleo.

Nadhani ifike wakati sasa tunaposema Mwanza ni jiji na kitovu cha biashara katika nchi za Afrika Mashariki basi hata mazingira yake yaendane lakini pia na watu waishi kwa masharti ya Jiji.

Viongozi wachukue jukumu la kukaa na wamiliki wote wenye vijumba hivi ambavyo vinatia doa jiji hilo waone namna ya kuondoa aibu hiyo na kuleta hadhi sawa na mategemeo ya walio wengi.

Ikiwezekana wawashauri waingine ubia na wenye uwezo wawajengee nyumba angalau zinazoendana na hadhi ya mji pengine kwa masharti maalumu.

Au ni vyema watu wakauza maeneo hayo kwa watu wenye uwezo wa kuyaendeleza na kuweka majengo bora halafu wao wakaenda kununua maeneo mengine ambayo wataweza kujenga nyumba zenye viwango sawa na uwezo wao.

Lakini kuendelea kukaa kama yalivyo hivi sasa ni kuonekana uchafu na takataka katikati ya mji.

Pia ifike hatua mamlaka ziweke utaratibu kwa nyumba kama hizo zipakwe rangi ili ziwe na mwonekano wa kisasa.

Jesse Mikofu ni mwandishi wa Mwananchi 0755996593